Wapenzi waperuzaji wa blogu yetu,
natumaini mmesherehekea vema sikukuu ya Krismasi na kuelekea mwaka mpya. Kwa
kuwa nimekuwa kimya kitambo kidogo si vema kama sitagusia kutoa salamu za pole
kwa msiba wa Shujaa Nelson Mandela. Hii inatokana na kuwa nje ya ofisi kwa
kipindi cha wiki tatu hivi. Kama nilivyoandika katika ukurasa wetu wa facebook
nampenda Thatha Mandela kwa jambo kubwa moja “ alifungwa gerezani kwa miaka
ishirini na saba, katika kipindi hicho alijifunza kusamehe na si kulipa kisasi”
kama dunia ingepata watu kama Mandela wenye moyo wa kusamehe hakika bara letu
lisingekuwa na migogoro mingi ya kisiasa kwani yote chanzo chake ni ubinafsi na
visasi. Kwa kuwa hiyo si habari yangu mahsusi kwa leo acha niifanye ya akiba
ili kuruhusu makala ya leo.
Mwishoni mwa mwaka tumeshuhudia
simanzi kubwa ikiibuliwa nchini baada ya kusomwa kwa ripoti Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili.
Nimejitahidi sana kujizuia nisiandike chochote juu ya Operesheni Tokomeza Ujangili lakini ghafla
nikajiwa na kumbukumbu mbaya za maangamizi ya wayahudi miaka ya 1940 kwenye
kambi SOBIBOR mpakani mwa Ujerumani na Poland. Operesheni iliyoongozwa na
dikteta Aldolf Hitler ama tunaweza kuyaita maangamizi ya karne iliutisha
ulimwengu, Ulaya hata Ujerumani yenyewe, ni mauaji yaliyoambatana na mateso
makali pamoja na matumizi ya gesi yenye sumu. Ndugu zangu Sobibor ilitisha
kwani vijana wenye nguvu walifanyishwa kazi ngumu zenye mateso makali hata
kufia kazini, watoto na wazee waliingizwa kwenye tanuru la moto na kuchomwa
humo. Maangamizi haya ya wayahudi wengi wasio na hatia yalifanywa na askari wa
Ujerumani kwa amri ya amiri jeshi mkuu wao Aldof Hitler katika kipindi cha vita
ya pili ya Dunia.
Ndugu zangu nimeanza kwa kugusia
tukio la kutisha la SOBIBOR baada ya kutafakari ripoti ya Lembeli na kupata
mrejesho mbalimbali kutoka kwa wabunge na watanzania. Ninajaribu kuitofautisha
Operesheni tokomeza Ujangili na maangamizi ya wayahudi kwa kuwa ni kama
vinafanana. Ndio kwani Operesheni hii askari walipohojiwa walisema wanatekeleza
agizo la Amiri Jeshi mkuu wakati Ujerumani pia ilikuwa kutii agizo la Amiri
jeshi Mkuu dikteta Adolf Hitler, Operesheni Tokomeza Ujangili ilifanywa na
jeshi la ulinzi na jeshi la polisi kadhalika maangamizi ya wayahudi.
Pamoja na ufanano huo lakini
nimebaini tofauti kubwa ya ile operesheni ya Hitler na hii ya vijana wa Mh.
Kikwete. Wakati ile ya Hitler ilitokana na chuki juu ya ustawi wa Wayahudi kwetu
Tanzania haikuwa hivyo bali ilikuwa chuki ya askari kwa watanzania tofauti
pasipo kujali rangi wala kabila, kila waliyemkumba walimuona ni jangili hata
kama anauza nyanya. Ukatili wa Operesheni hii ni mbaya haijawahi tokea, kwani
ni zaidi ya vita maana nijuavyo katika vita husikika milio ya risasi askari huua
ili kusonga mbele. Lakini katika Operesheni hii askari walipiga kambi katika
vijiji wakakamata watu na kuanza kuwadhalilisha, udhalilishaji wa hali ya juu,
wengine waliwatesa ili mradi vurumai. Hapo ndo huwa nachanganyikiwa kwamba
askari hawa walikuwa na chuki na nani na kwa sababu gani? Wajipambanue kwani
Ujerumani walijitambulisha wazi kuwa walikuwa na chuki na wayahudi. Sielewi
kama taaluma yao ina mapungufu makubwa hata kutoweza kubaini wahalifu hivyo
kuamua kusomba kila waliyemuona, na hata walipoamua kuwasomba je hawaelewi
katiba inasemaje juu yao? Hakuna mahakama hata wakageuka wao askari na tena
mahakimu wakiwahukumu watu kwa adhabu kali hata kuwaua? Je askari hawa walikuwa
wanatekeleza agizo la nani? Maana amiri jeshi mkuu Mh Rais Kikwete hakusikika
akiagiza wakaue, wakadhalilishe na kuwatesa watanzania au labda kwa kuwa waziri
Kagasheki alisema ikiwezekana majangali yauawe hukohuko?
Jaman watanzania tumefikia huko? Sasa
nababaika ikiwa wanajeshi wanaoiwakilisha nchi huko Lebanon, Sudani na Kongo
kama wanatuwakilisha vema kwani ikiwa watanzania wenzao wanawatenda hivi je hao
wa huko si mara mia? Hebu tuangalie sehemu ya ripoti inapoonyesha udhalilishaji
uliotokea.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo, James Lembeli akisoma ripoti hiyo bungeni alisema Operesheni
Tokomeza Ujangili, ulisababisha hofu miongoni mwa wananchi na viongozi na
baadhi yao kuyakimbia makazi. Lembeli alisema watuhumiwa, walikamatwa,
walipekuliwa na kudhalilishwa na baadhi kutojulikana walipo.
“Baadhi ya
wananchi wakiwemo viongozi, madiwani na wenyeviti wa vijiji na vitongoji na
watumishi wa Serikali, walikamatwa na kudhalilishwa mbele ya wananchi
wanaowaongoza,” alisema Lembeli
Aliongeza;
“Watuhumiwa waliokamatwa walidai kudhalilishwa mbele ya wanafamilia kwa kupewa
adhabu wakiwa uchi na wanawake kushikwa sehemu za siri bila ridhaa yao.”
Lembeli
alitoa mfano kuwa Ali Nyenge (38) wa Kata ya Iputi, Wilaya ya Ulanga alidai
kuvuliwa nguo, kumwagiwa maji yaliyochanganywa na chumvi na kuchapwa viboko
huku mwanawe wa kiume (11) akishuhudia huku akilazimishwa kuchora picha ya
Chatu kwa kutumia wembe kwenye paja lake.
Alisema
mwanamke mmoja wa Babati (jina tunalo) alidai kuvuliwa nguo na
kulazimishwa kufanya mapenzi na wakwe zake, pia kuingizwa chupa sehemu zake za
siri.
Aidha,
baadhi ya wanawake walidai kubakwa na kulawitiwa huku wilayani Ulanga, mwanamke
mmoja alidai kubakwa na Askari wawili wa Operesheni Tokomeza Ujangili mida ya
usiku.
Hivi kama
Operesheni hiyo ingeendelea japo kwa mwaka mmoja ingekuwaje? Si ni zaidi ya
SOBIBOR maana ya Hitler hatukusikia ubakaji, kulazimisha wakwe kufanya mapenzi,
hatukusikia uingizaji wa chupa, kujichora kwa nyembe mwilini na mateso mengi
kama yaliyofanywa katika operesheni hiyo. Hakika haifanani hata kidogo.
Hebu tazama
baadhi ya picha na video zikionyesha sehemu ya Operesheni hiyo;
Hii ndio
moja ya unyama uliofanyika kwenye Operation Tokomeza Ujangili iliyosimamiwa na
washiriki toka Wizara 4 za mawaziri waliondolewa juzi bungeni.

Japo ripoti hiyo imesababisha
mawaziri wanne kutenguliwa uteuzi wao lakini kwa nchi yetu ambayo inaiangaza
Afrika na Dunia nzima kwa mwenge wake juu ya Mlima Kilimanjaro, inatupasa
kwenda mbali kuwakabili wote waliojaribu kuichafua nchi yetu waliothubutu
kuondoa amani kwa raia wasio na hatia. Kila aliyehusika katika operesheni hiyo
si tu afukuzwe kazi kuwafuata wakubwa zake mawaziri waliofukuzwa, la hasha wataendelea kutamba mtaani bali
wakamatwe wapelekwe mahakamani wakashtakiwe ili wajue ni nchi inayoendeshwa kwa
mujibu wa katiba na si wahuni na wababe wachache.
Hapa natamani kuzichochea taasisi
zinazoweza kusisitiza haki kutendeka, yaani vyama vya siasa, tume ya haki za
binadamu na wanaharakati mbalimbali kupaza sauti zao katika hili kwani likipita
kimya kwa kuwawajibisha mawaziri tu linaweza kujirudia na kuwa baya zaidi.
Wahenga walisema Hala hala Mti na
Jicho.
No comments:
Post a Comment