m

"If you want to conquer fear, don't sit at home and think about it. Go out and get busy. "

-- Dale Carnegie, motivational expert

Sunday, 2 June 2013

Mauaji ya kutisha yaibuka msituni

 
Na Burhani Yakub,Horohoro  (email the author)

Posted  Juni1  2013  saa 20:14 PM
Kwa ufupi
  • Kwa kipindi kirefu msitu huo umekuwa eneo la kufanyia mauaji kwa watu wasio na hatia, ambapo genge la wahalifu kutoka Kenya limedaiwa kuhusika na mauaji hayo.

Matukio ya mauaji ndani ya msitu wa Mwakijembe yameendelea kutishia usalama wa Watanzania, wanaoishi jirani na eneo la Horohoro linalopakana na nchi jirani ya Kenya.
Kwa kipindi kirefu msitu huo umekuwa eneo la kufanyia mauaji kwa watu wasio na hatia, ambapo genge la wahalifu kutoka Kenya limedaiwa kuhusika na mauaji hayo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini msitu huo wenye rasilimali nyingi unaodaiwa kutumiwa na genge hilo kwa vitendo haramu vya ujangili, uchimbaji madini na uvunaji wa miti, ikiwemo uchomaji mkaa.
Taarifa za uchunguzi ambazo zilithibitishwa na viongozi wa Serikali ya Vijiji vinavyopakana na msitu huo, zilibaini genge hilo limekuwa likiua kila linayemhisi atafichua uhalifu wao.
Inatoka UK 1
Uchapisha wa Hati za Kusafiria (Kwa mujibu wa taarifa za karibuni, kwa mwaka huu pekee, watu wawili tayari wameshauawa kwa kuchinjwa ndani ya msitu huo.
Matukio hayo ya mauaji yalithibitishwa na Diwani wa Kata ya Mwakijembe, Ramadhani Mtiota ambaye alisema kwa sasa katika eneo hilo hali imekuwa ya hofu kutokana na kuongezeka kwa makundi ya vijana wa rika la Morani wa Kimasai, wanaojiandaa kuvishambulia vijiji vya Kenya.
Diwani huyo alisema ametoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza kuhusu hali hiyo pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Andrew Ngoda.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alisema wanafahamu kuhusu mauaji yanayotokea kwenye msitu huo.
Alisema taarifa za mauaji ya hivi karibuni ya watu wawili, Ali Mohamed na msichana wa kabila la Kimasai Kendie Minja yanafahamika na yanafanyiwa uchunguzi na polisi.
”Ninachofahamu ni mauaji yaliyofanyika ya msichana Kendie kuchinjwa na kufichwa msituni upande wa Kenya, lakini upelelezi unafanywa na Jeshi la Polisi la wenzetu wa Kenya kwa hivyo sijui zaidi ya hivyo,” alisema Massawe.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza alisema anaandaa mkutano wa ujirani mwema utakaowahusisha viongozi wa Serikali Mkoa wa Tanga na Jimbo la Mombasa, Kenya.
http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Mauaji-ya-kutisha-yaibuka-msituni/-/1597296/1869732/-/11tcb6hz/-/index.html 

Membe: Tanzania haiwezi kuomba radhi Rwanda

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akipongezwa na Mawaziri na wabunge mara baada ya kusoma makadirio ya bajeti ya wizara yake Bungeni. ameelezea  kuwa Tanzania haitaiomba Rwanda msamaha kutokana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete 
Na Fidelis Butahe, Mwananchi  (email the author)

Posted  Juni1  2013  saa 20:22 PM
Kwa ufupi
  • Serikali ya Rwanda iliitaka Tanzania iombe radhi kwa madai kuwa kauli ya Rais Kikwete ni kama tusi kwao na kwamba wao hawawezi kukaa na kuzungumza wapinzani ambao ni wauaji

Dodoma. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema kamwe Tanzania haitaiomba radhi Rwanda, baada ya Rais Jakaya Kikwete kuishauri nchi hiyo kufanya mazungumzo na upinzani ili kumaliza vita katika eneo hilo la Maziwa Makuu.
Serikali ya Rwanda iliitaka Tanzania iombe radhi kwa madai kuwa kauli ya Rais Kikwete ni kama tusi kwao na kwamba wao hawawezi kukaa na kuzungumza wapinzani ambao ni wauaji.
“Kama Rwanda haitaki kufuata ushauri wa Rais Kikwete inatakiwa kuuacha na siyo kumtaka aombe radhi,” alisema.
Membe alitoa ufafanuzi huo bungeni jana wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge katika mjadala wa makadirio ya matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka 2013/2014.
Tamko hilo la Serikali limekuja ikiwa zimepita takriban siku sita tangu Serikali ya Rwanda kutoa tamko la kupinga ushauri huo uliotolewa na Rais Kikwete wakati akiwa katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Akijibu pendekezo hilo la Rais Kikwete, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo alisema kuwa Rwanda haiko tayari kufanya mazungumzo na watu ambao walishiriki kwenye mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, dhidi ya Watutsi na kwamba kufanya hivyo ni sawa na kuhalalisha mauaji kwa wananchi wake.
“ Wale wote wanaodhani kuwa Rwanda itaanzisha majadiliano na waasi wa FDLR nadhani kwa ukweli hawajui kile wanachozungumza. Rwanda haiwezi kujadiliana na wauaji,” alisema waziri huyo wakati akizungumza na Idhaa ya Kimataifa ya Radio Ufaransa.
Alisema kuwa wakati serikali ya Rwanda imefaulu kuzika mienendo inayopalilia mauaji ya halaiki, lakini bahati mbaya kumesalia makundi ya watu ambayo bado yanahubiri itikadi zinazokumbusha uchungu na kutonesha kidonda kilicholeta maafa makubwa kwa wananchi.
“ Kumbe kuna wasemaji wengi wa kundi la FDLR. Wengine wao wanaendelea kufungamana na itikadi za kundi hili. Rwanda ilifaulu kutokomeza mauaji ya halaiki lakini hatukutokomeza itikadi za kundi hili,” alisema waziri huyo.
Kauli ya waziri huyo imeungwa mkono na baadhi ya wasomi pamoja na wanaharakati waliosema kuwa kuiomba Rwanda ianzishe majadiliano na kundi hilo, wanapaswa kufikiri mara mbili.
Katika ufafanuzi wake Membe alimnukuu Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Isaack Rabin kwamba mwaka 1995 aliwahi kutoa tamko lililosema, ‘Tunajenga amani na tunajadiliana na maadui zetu na si marafiki’.
Alisema kama Serikali ya Rwanda itakuwa imesikia kauli hiyo inatakiwa kufanya mazungumzo ya amani na maadui, na wasingoje kufanya mazungumzo ya amani na Tanzania, ambayo wana uhusiano mzuri na ni nchi rafiki kwa muda mrefu.
http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Tanzania-haiwezi-kuomba-radhi-Rwanda/-/1597296/1869740/-/11cm237z/-/index.html