Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
amezindua jumba jipya makao makuu ya Umoja wa Afrika ambalo limepewa
jina la rais mwanzilishi wa taifa la Tanzania, Julius Nyerere.
Jumba hilo ambalo jina lake kamili ni Jumba la Amani na Usalama la Julius Nyerere limejengwa kwa ufadhili kutoka Ujerumani.
Litakuwa
makao ya idara ya Amani na Usalama ya AU na litatumiwa pia na maafisa
wa kutoa tahadhari ya mapema kuhusu mizozo barani pamoja na kuratibu
juhudi za kulinda amani za AU.
Ujenzi wa jumba hilo, ambalo ukubwa
wake wa sakafu ni mita 13,500 mraba na linaweza kutumiwa na wafanyakazi
360, uligharimu euro 27 milioni.
Jumba hilo afisi za kufanyia
kazi, vyumba vya mikutano vya kutumiwa na Baraza la Amani na Usalama,
chumba cha kuratibia shughuli, maktaba na vyumba vya shughuli za
pembeni.
Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa rais wa Tanzania hadi
1985, alikuwa mmoja wa viongozi waanzilishi wa Muungano wa Nchi za
Afrika (OAU) ambao sasa ni Umoja wa Afrika (AU).
Alishiriki sana katika jitihada za kuendeleza bara
la Afrika na kusaidia mataifa ambayo hayakuwa yamepata uhuru kujipatia
uhuru wake.
Mwalimu Nyerere alipigania sana kumalizwa kwa ubabe wa
Wazungu katika nchi za Rhodesia (sasa Zimbabwe), Afrika Kusini, na
taifa la Kusini Magharibi mwa Afrika/Namibia (sasa Namibia).
Source:BBCSwahili