Matokeo ya kidato cha nne kwa mara
nyingine yamekuwa mabaya na mabaya zaidi ukilinganisha miaka mingine, wengine
wameyaita bomu japo binafsi sioni kama ni bomu nahisi ni moshi tu mlipuko
wenyewe bado. Naeleza hivi kwa sababu bado kuna kila dalili ya bomu lenyewe
yaani tutegemee matokeo mabaya zaidi ikiwa hatua hazitachukuliwa. Ukirejelea
makala yangu ya mwaka jana (2012) yenye kichwa Unahitajika Utafiti wa Kina Juu
ya Ufaulu wa Wanafunzi inayopatikana http://kapagiii.blogspot.com/search?updated-min=2012-03-01T00:00:00-08:00&updated-max=2012-04-01T00:00:00-07:00&max-results=2
ilieleza wazi walengwa sita wanaopaswa kutazamwa juu ya matokeo ya kidato cha
nne. Nitawaorodhesha kwa ufupi uwezo wa wanafunzi wenyewe (personal ability),
Mzazi wa mwanafunzi, mwalimumazingira ya elimu na shule zenyewe, jamii yote kwa
ujumla na mwisho serikali na vyombo vyake muhimu vya elimu, wizara, Taasisi ya
Elimu Tanzania.
Nasikitika kuwa matokeo ya mwaka 2011
licha ubovu wake hakuna utafiti wowote hata ripoti ya nini kilisababisha na
matokeo yake ndo haya matokeo yenye kuvunja rekodi. Nashukuru sasa kumeundwa
tume, nikitazama wajumbe wa tume napata tumaini ninapoona jina la Rakesh Rajan
katibu mtendaji wa Twaweza ambao wanajihusisha sana na utafiti wa elimu ukiwemo
ule wenye kichwa “Are Our Children Learning” wa mwaka 2010 ambao binafsi
nilipousoma nilibaini matatizo makubwa katika elimu yetu lakini cha ajabu
utafiti wako haukutiliwa mkazo na serikali yetu. Serikali yetu ni bingwa wa
kutupa mafaili ya utafiti na ripoti mbalimbali pasipo kujali gharama na faida
yake. Prof. Kezilahabi katika riwaya yake ya “Nagona” ya mwaka 1978 anajaribu
kueleza hili anapoonyesha mafaili ya utafiti yakiwa yametupwa jaani. Chonde ripoti itakayopatikana kutokana na
tume hii itendewe kazi ikiwa tunataka kuliokoa Taifa hili la sivyo bomu kubwa
litapuka.
Pamoja na matokeo hayo binafsi nakumbuka
umuhimu wa vyuo vya maendeleo ya jamii (FDC) na vyuo vya ufundi. Kundi hili
kubwa la watoto waliofeli cha kusikitisha ni kuwa haliwezi kujitegemea na hivyo
kama tungekuwa na vyuo vya maendeleo ya jamii na hata vya ufundi vya kutosha
vingesaidia kupunguza mzigo huu. Inasikitisha kuona vyuo hivyo havikuendelezwa
na hata vilivyopo vipo katika hali mbaya, kwa mifano hai unaweza kutembelea
FDC- Katumba(Tukuyu), FDC-Bigwa (Morogoro), FDC- Uyole (Mbeya) na FDC-Kibaha
(Pwani) vyote vinatapatapa katika hali mbaya kabisa. Kama kundi hili lililofeli
halitapatiwa ujuzi wowote litaleta shida baadaye kwani hata Johannesburg ule
mji wa pili kwa uhalifu duniani umesababishwa na vijana waliokosa tumaini la
maisha baada ya kukosa elimu. Japo elimu hii ya ufundi inadharauliwa lakini
ikumbukwe kuwa ndiyo iliyowakomboa wachina na sasa wanatamba maendeleo ya
sayansi na teknolojia.
Nimalize kwa kusisitiza serikali kuchukua
hatua za maksudi katika elimu na pia kuangalia vyuo vya maendeleo ya jamii na
vyuo vya ufundi ili watoto wanapofeli wasiachwe tu bali wapate elimu ya ufundi,
na wanafunzi wawe tayari kuipata ikiwa ni pamoja na wazazi kutoa ushirikiano wa
dhati. Kwa pamoja tunaweza kuikomboa nchi yetu.
Wenu
Peter
Kapagi
SJUT-Dar
es Salaam
Simu
ya kiganjani; +255 764 734620