m

"If you want to conquer fear, don't sit at home and think about it. Go out and get busy. "

-- Dale Carnegie, motivational expert

Thursday, 16 May 2013

Tume ya Kidato cha IV yatoa mapendekezo 130

 
Profesa Sifuni Mchome 
Na Fredy Azzah, Mwananchi  (email the author)

Posted  Jumanne,Mei14  2013  saa 20:25 PM
Kwa ufupi
  • Pendekezo la kufutwa kwa matokeo na kisha kupangwa upya ni moja tu kati ya mengi. Mpaka sasa tumeandaa zaidi ya mapendekezo 130 na kazi bado inaendelea

Dar es Salaam. Tume ya Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha Ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012, imetoa mapendekezo 130, mojawapo ikitaka kupitiwa upya kwa mitalaa ya elimu nchini.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Profesa Sifuni Mchome alisema likitaka mitalaa ya shule za msingi hadi vyuo vya ualimu itazamwe upya.
Tume hiyo iliundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Februari 23, mwaka huu kuchunguza chanzo cha asilimia 65.5 ya wanafunzi kupata daraja la sifuri kwenye mtihani wa mwaka 2012.
Alisema mapendekezo hayo yatawasilishwa kwa Waziri Mkuu baada ya Tume kumaliza kazi yake Juni 15 mwaka huu.
“Pendekezo la kufutwa kwa matokeo na kisha kupangwa upya ni moja tu kati ya mengi. Mpaka sasa tumeandaa zaidi ya mapendekezo 130 na kazi bado inaendelea,” alisema Profesa Mchome.
Alisema kwa kawaida mtalaa unabadilishwa baada ya kumaliza mzunguko wake mmoja, hivyo tume hiyo imependekeza kupitiwa upya kwa mitalaa yote ambayo imemaliza mzunguko. Mzunguko huu ni miaka saba kwa elimu ya msingi, minne kwa sekondari na miwili kwa kidato cha tano na sita.
“Mtalaa wa sekondari unaweza kupitiwa upya baada ya miaka minne tangu kuanza kutumika kwake, huu wa Sekondari wa ‘based competence’ (kuangalia ubora) ulianza kutumika 2006, mpaka sasa tayari umemaliza mzunguko wake na haya matokeo yametokana na mtalaa huu.
Tume imependekeza mitalaa yote itazamwe upya kuanzia ile ya shule za msingi mpaka vyuo vya ualimu,” alisema.
Kuhusu vitabu, Tume imependekeza kuangaliwa kwa njia rahisi ya kutumia teknolojia kuhakikisha vinapatikana badala ya kusubiri mpaka vichapishwe na kisha kupelekwa kwa wanafunzi.
“Unaweza ukaongea na makampuni ya simu kuwa waweke vitabu kwenye system (mfumo) yao na wakaanza mashindano kuwa mwanafunzi atakayesoma sana atapata zawadi,” alisema na kuongeza.
“Unaweza pia kuongea na kampuni ya magazeti kama Mwananchi ukawaambia watoe ukurasa wachapishe kitabu fulani kwa mwezi mzima na shule ziambiwe zinunue nakala moja ambayo kwa mwezi itakuwa Sh30,000 kwa kila shule na tatizo la vitabu litakwisha.”
Pendekezo jingine alisema ni kuangaliwa upya kwa sheria mbalimbali za elimu jinsi zilivyo na utekelezwaji wake pamoja na kuhakikisha madaraka yanapelekwa kwenye ngazi za Serikali za Mitaa.
http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Tume-ya-Kidato-cha-IV-yatoa-mapendekezo-130/-/1597296/1852852/-/12p5ogez/-/index.html

Hayati Patrice Lumumba atunukiwa mji


Lumumba alichaguliwa kama waziri mkuu wa DRC mwaka 1960
Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo inatarejiwa kujenga mji ambao utakuwa kumbukumbu na kwa mpiganiaji uhuru wa nchi hiyo Patrice Lumumba . Hii ni kwa mujibu wa msemaji wa serikali Lambert Mende.
Lumumba aliongeza kuwa, mji huo utakaojulikana kama Lumumbaville utazileta pamoja jamii mbili zilizoko katika eneo hilo.
Lumumba aliyekuwa mshirika wa nchi za muungano wa Kisovieti, alichaguliwa kama waziri mkuu mwaka 1960, baada ya zaidi ya karne moja ya utawala wa kikoloni.
Mauaji yake, yalitokea miezi minne baadaye alipokuwa na umri wa miaka 35 na Marekani na Uingereza ndizo zililaumiwa kwa kifo chake.
Mwezi Aprili, mmoja wa wabunge wa bunge la malodi nchini Uingereza alisema kuwa afisaa mmoja wa MI6, alimwambia kuwa Uingereza ilihusika na kifo cha Lumumba.
Mwandishi wa BBC mjini Kishansa anasema kuwa habari hii bila shaka itapokelewa vyema na wananchi wa DRC kwani Lumumba anasalia kuwa mtu mashuhuri.
Mji wa Lumumbaville utajengwa katika mkoa wa Kassai-Oriental ambako alizaliwa hayati Lumumba.
Ujenzi wa mji huo unatarajiwa kuanza mwaka 2014, aliongeza kusema bwana Mende.
Serikali inatumai kuwa wahisani watasaidia katika ujenzi wa mji huo na kuwa utakuwa kivutio kwa watalii.
Mwanawe Lumumba, Raymond, aliambia BBC kuwa babake angefurahia sana uamuzi wa serikali kujenga mji huo.
"alitaka Congo kuwa kitovu cha maendeleo barani Afrika," alisema Raymond Lumumba.
"kwa hivyo, angetaka uwe mji wa kisasa.''
DR Congo ina utajiri wa madini ingawa watu wengi wanaishi katika umaskini.
Nchi hiyo imekumbwa sana na mizozo kadha wa kadha tangu ijipatie uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.
Mzozo wa hivi sasa ambao umesababishwa na kundi la M23, ulianza mwaka jana Mashariki mwa nchi na kusababisha takriban watu 800,000 kutoroka makwao.
chanzo; bbcswahili.com