
Chacha Makenge akitoka kwenye handaki lake. Picha na Florence Majani.
Na Florence Majani, Mwananchi
- Aliwahi kulazwa wodi ya wagonjwa wa akili Muhimbili
Tunaposikia handaki, fikra zinatupeleka moja kwa
moja kwenye vita kwani aghalabu, mahandaki hutumiwa na watu kujificha
wakati wa vita.
Hata hivyo, ugumu wa maisha umesababisha baadhi ya watu kuyageuza mahandaki kama makazi ya kuishi.
Ni katika Barabara ya Sam Nujoma, natoka Ubungo
kuelekea Mwenge, nashuka mita chache kabla ya kufika Mlimani City,
naingia katika pori lililo nyuma ya Ukumbi wa Mlimani City.
Hakuna njia maalumu ya kuingia katika pori hili.
Hatua kwa hatua napita katikati ya vichaka na nyasi ndefu, hatimaye
nafika katika eneo tofauti. Ni kama bustani iliyotengenezwa na mbunifu
wa hali ya juu.
Miti imefyekwa kwa utalaamu wa hali ya juu,
baadhi ya vichaka vimepunguzwa kwa umahiri na kutengeneza umbile zuri
mfano wa maua yaliyotengenezwa. Lakini, mwisho kabisa wa mandhari hii
kuna mianzi imelazwa chini na pembeni kuna shimo.
Shimo hilo ndilo handaki analoishi Chacha
Makenge, kijana mwenye umri wa miaka 36, mzaliwa wa Mugumu Wilaya
Serengeti Mkoa wa Mara kwa muda wa miaka minne sasa.
Hata hivyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Profesa Makenya Maboko anasema kuwa hana taarifa zozote kuhusu
Makenge kuishi katika eneo hilo.
“Sina taarifa, wewe ni mtu wa kwanza unanipa habari hizi, ngoja nilifanyie kazi,” anasema Profesa Maboko.
Jirani na handaki hilo namkuta Makenge akifyeka
majani kwenye bustani yake. Ananikaribisha na tunaingia katika handaki
hilo. Ni shimo refu, kwani tunatakiwa kushuka ngazi tatu kubwa kwenda
chini. Ndani kuna kitanda cha kamba na miti kilichofunikwa kwa magunia
na shuka kadhaa.
Ukuta ambao ni udongo, umechongwa mithili ya meza
ndogo ambayo Makenge ameweka kioo, kitana, boksi lenye dawa mbalimbali
na mswaki.
Upande wa kulia wa handaki hili kuna misumari
iliyopigiliwa katika ukuta huo ambapo Makenge ametundika makoti na
suruali, ambazo bila shaka ni zake.
Upande wa kushoto, Makenge kwa kutumia ukuta huo
huo, ametengeneza meza nyingine ambayo imewekwa chupa za plasitiki za
maji ya kunywa.
soma zaidi kwa kubofya hapa http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Aishi-kwenye-handaki-kwa-miaka-minne/-/1597296/2120902/-/11ifsp3z/-/index.html
soma zaidi kwa kubofya hapa http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Aishi-kwenye-handaki-kwa-miaka-minne/-/1597296/2120902/-/11ifsp3z/-/index.html
No comments:
Post a Comment