
Abiria wakigombea basi dogo katika kituo cha mabasi ya daladala Ubungo jijini Dar es Salaam jana.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa maeneo ambayo
yamekumbwa zaidi na tatizo la usafiri ni kutoka Mwenge kwenda Tegeta,
Mwenge-Kibaoni, Ubungo-Mbezi, Ubungo-Mbagala, Gongolamboto-Mwenge na
Ubungo kwenda Mlandizi.
Kutokana na ukosefu wa daladala kwenye maeneo hayo, kwa takribani
wiki moja sasa wananchi wamekuwa wakitumia malori, Toyota Noah, Bajaj,
Pick Up, teksi pamoja na Toyota Coaster ambazo hazijasajiliwa kuchukua
abiria jijini hapa.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa kutokana na ukosefu wa daladala, hali
hiyo imetoa fursa kwa magari yaliyoanza kutoa huduma ya usafiri kwenye
maeneo hayo kutoza abiria nauli kubwa ambayo haipo katika viwango vya
nauli vilivyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Usafiri wa
Majini na Nchi kavu (Sumatra). Nauli inayotozwa na wamiliki magari hayo
mfano kutoka Mwenge hadi Tegeta, Mwenge-Bunju, Mwenge-Kibaoni ni
Sh.1,000 hadi 2,000 kwa mtu mmoja badala ya Sh. 300 au 400 ya sasa.
Kutoka Ubungo kwenda Mbezi, Ubungo-Mbagala, nauli zinazotozwa ni
kati ya Sh. 500 hadi 1,000 badala ya Sh.300 wakati kutoka
Ubungo-Mlandazi ni Sh.1,000 hadi 2,500.
Magari yaliyobainika kutoza nauli kubwa ni yale ambayo
hayajasajiliwa na Sumatra kutoa huduma ya usafiri katika Jiji la Dar es
Salaam na yaliyoiba njia.
Aidha, daladala ambazo zimesajiliwa kutoa huduma jijini hapa,
zinaongoza kukatisha ruti (kuiba njia) na zinafanya hivyo ziweze kurejea
mapema vituoni kuchukua abiria wengine hali ambayo inakuwa ni faida
kwao.
Mathalani, katika kituo cha Mwenge inapofika jioni, gari za ruti ya
Tandika-Mwenge kupitia barabara ya Ali Hassan zimekuwa zikipakia Ubungo
na kisha kushusha abiria wote na kupakia tena kwenda Bugurudi na
zinapofika hapo hupakia kwenda Tandika.
Wakati mwingine, gari hizo zinapofika Ubungo hurudi tena Mwenge kupakia abiria.
Wakizunguma na NIPASHE kituo cha Ubungo, abiria waliokuwa
wakisafiri kwenda Mbezi Luis, walisema tatizo la usafiri limekuwa sugu
na kwamba wakati mwingine wanachukua zaidi ya saa tano kupata gari.
Amon Kisimbo mkazi wa Mbezi Luis alisema tatizo la usafiri katika
jiji la Dar es Salaam linasababishwa na msongamano wa malori na kwamba
serikali inatakiwa kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyowahi kutolewa mwaka
2009.
Kisimbo ambaye alidai alikuwa miongoni mwa watu walioshiriki
kuandaa mapendekezo hayo katika tume iliyoundwa na serikali, alisema
pendekezo walilotoa ni kutaka Bandari ya Dar es Salaam ihamishwe kutoka
ilipo sababu inasababisha malori kupita katikati ya jiji na hivyo
kusababisha msongano usiokuwa wa lazima. Ofisa Mfawidhi wa Sumatra,
Kanda ya Mashariki, Conrad Shio, akizunguza na NIPASHE jana alisema
kutokana na ukiukwaji wa sheria za barabara unaofanywa na wenye magari
hayo, magari 74 yamekamatwa kutokana na makosa mbalimbali.
Shio alisema magari 36 yamekamatwa kwa kukatisha ruti, 18 kwa kuiba ruti na magari 20 yamekamatwa kwa kutoza nauli kubwa.
Alisema magari ambayo yamekamatwa kwa kosa la kukatisha ruti
wamiliki wake watatakiwa kwenda Sumatra na mkataba wa madereva wengine
na hao waliosababisha kosa hilo hawataruhusiwa kufaya kazi ya udereva
mahali popote nchini.
Alisema tatizo la ukosefu wa magari katika baadhi ya maeneo
linatokana na kwamba Sumatra imesimamisha usajili katika ruti ya
barabara ya Ali Hasani Mwinyi-Kilwa kwa sababu kuanzia Julai mwaka huu
wamiliki wa daladala watatakiwa kujiunga katika kampuni ili kutoa huduma
ya usafiri kwenye ruti hiyo.
Alisema siyo kweli kwamba daladala zimeadimika na kwamba baadhi ya
wamiliki wanakwepa kusajili magari yao kwenye njia zenye foleni kubwa
kama Mbezi-Kimara hadi Kivukoni au Kariakoo.
MWAKYEMBE ABARIKI NAULI
Serikali imebariki ongezeko jipya la nauli za mabasi yanayotoa
huduma mijini, ya masafa marefu na treni hivyo kuziruhusu kuanza
kutumika rasmi leo.
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, aliwaambia wanahabari
jana mjini Dodoma kuwa nauli mpya imeongeza Sh. 50 kwa mwanafunzi na Sh.
100 kwa watu wazima; hivyo daladala zitatoza Sh. 400 badala ya 300 na
wanafunzi Sh. 200 badala ya Sh. 150.
Alisema serikali imeridhia ongezeko la nauli lililotangazwa na
Sumatra, baada ya kuhakiki na kujiridhisha kuwa ongezeko hilo
lilizingatia mchakato wa kupandisha nauli na viwango viliridhiwa na
wadau wanaowakilisha maslahi ya wanaotoa na wale wanaotumia huduma hiyo.
“Mimi kama Waziri wa Uchukuzi sina tatizo na ongezeko hili dogo la
nauli za daladala tatizo langu ni tabia ya Watanzania kukacha vikao
halali vinavyojadili mambo yanayotuhusu na kusubiri kuja kulalamika
baadaye,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema hayo akiwakosoa wananchi na asasi nyingine kulalamikia
nauli nje ya utaratibu licha ya vikao vya kuwataka kutoa maoni kupitia
Sumatra kutangazwa na kuwataka wananchi wajitokeze wakati maombi ya
wamiliki wa vyombo vya usafiri ya kupandisha nauli yalipokuwa
yanajadiliwa.
Waziri Mwakyembe alisema maombi ya kuongezwa nauli hiyo mpya
yalitolewa baada ya wadau wakiwamo Baraza la Taifa la Walaji wa Huduma
zinazodhibitiwa na Sumatra, Chuo cha Usafirishaji, vikiwamo vyama vya
watoa huduma vya madereva vya kutetea abiria na wanahabari, kuridhia.
“Kulikuwa na mvutano mkubwa wamiliki wakitaka nauli iongezeke na
wawakilishi wa abiria wakitaka nauli ibakie ile ile iliyotangazwa mwaka
2011. Ndipo maamuzi ya nyongeza ya nyongeza ndogo yakawa Sh. 100 na Sh.
50 kwa mwanafunzi yakaafikiwa,” alisema.
Aliongeza kuwa wawakilishi wa abiria na wamiliki wa vyombo vya
usafirishaji waliamriwa kuwa iwapo kuna upande usioridhia ukate rufaa
kwenye Baraza la Ushindani, lakini hakuna aliyefanya hivyo.
Wiki iliyopita Waziri Mwakyembe alisema wizara hiyo itapitia nauli
hizo kutokana na malalamiko mengi kutolewa na wananchi wakipinga
nyongeza hiyo.
Imeandikwa na Gaudensia Mngumi, Dodoma na Thobias Mwanakatwe, Dar
CHANZO:
NIPASHE