Katika kikao cha Kamati Kuu ya
CHADEMA kilichofanyika tarehe 20-22 Novemba 2013, pamoja na mambo
mengine, kulijadiliwa waraka wa siri unaojulikana kama Mkakati wa Mabadiliko
2013. Waraka huu ulilenga kujenga hoja ya kufanya mabadiliko ya uongozi na
kuanisha mikakati ya ushindi kwa mgombea mlengwa katika uchaguzi mkuu ndani ya
CHADEMA. Nilikiri kuwa nilikuwa naufahamu waraka huu, na kwamba nilishiriki
kuuandaa na kuuhariri, na kwamba mimi ni mmoja wa wanachama wanaoamini kwamba
kuna haja ya kubadilisha uongozi wa juu wa chama katika uchaguzi ujao ndani ya
chama.
2.
Katika mjadala, maudhui ya waraka
huu yalionekana kwa wajumbe kwamba yalikuwa na mapungufu na yalikiuka misingi
na kanuni zilizoanishwa katika Katiba ya Chama. Kwa kuwa katika chama cha siasa
hoja za watu wengi ndizo hupewa uzito, na kwa kuwa dhamira na nia yangu ndani
ya chama hiki imekuwa ni kusukuma mabadiliko ambayo watanzania wanayatazamia
nje ya mfumo wa sasa wa utawala, nilikiri makosa yangu na kuwaomba msamaha
wajumbe wa Kamati Kuu na viongozi wakuu wa chama, na kueleza kwamba nilikuwa
tayari kujiuzulu na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida. Wajumbe walikataa
kukubali ombi langu la kujizulu bali walipitisha azimio la kunivua mimi na Mhe.
Zitto Zuberi Kabwe nafasi zetu za uongozi. Nilipokea kwa unyenyekevu adhabu ya
kuvuliwa nafasi zote za mamlaka nilizokuwa nazo ndani ya chama hiki na kueleza
kuwa nitaendelea kutoa mchango wangu kama mwanachama wa kawaida hadi hapo chama
kitakapoona ninafaa kukitumikia katika nafasi yeyote.
3.
Kufuatia mkutano wa waandishi wa
habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013 ambapo, pamoja na mambo mengine,
ilielezwa na viongozi wa CHADEMA kwamba mimi na wenzangu (Samson Mwigamba na
Zitto Kabwe) tumehujumu chama na tumefanya uhaini kwa kuandaa mkakati wa
ushindi kwa mgombea tunayemtaka, ningependa nieleza mambo yafuatayo:
a.
Siamini hata kidogo kwamba kugombea
nafasi yeyote iliyo wazi ndani ya chama cha siasa ni uhaini na hujuma. Msingi
namba moja wa CHADEMA ni demokrasia na hakuna namna ya kudhihirisha mapenzi kwa
demokrasia zaidi ya kuruhusu ushindani katika nafasi za uongozi na hasa uongozi
wa juu kabisa. Hiki kinachoitwa uhaini ni wasiwasi wa siasa za ushindani
katika chama chetu.
b.
Sijawahi na sitarajii kushiriki
vitendo vyovyote vya kuhujumu chama changu cha CHADEMA na harakati za
mabadiliko hapa nchini. Chama hiki kiliniamini katika nafasi nyingi nyeti sana
na kama mie ningekuwa mhujumu nilikuwa na fursa nzuri za kufanya uhujumu huo.
Nimeshiriki kuandaa ilani ya chama ya 2010-2015, kuratibu kampeni za mwaka 2010
nikiwa makamu mwenyekiti wa kampeni chini ya Profesa Baregu na nilishiriki
kutengeneza na kusimamia utaratibu mzuri wa kupata wabunge wa viti maalumu
katika chama chetu. Zote hizi ni nafasi nyeti mno ambazo kamwe huwezi
kumkabidhi mtu ambaye ni ‘mhaini’ na ‘mhujumu’. Nilishiriki katika
shughuli za chama kwa kiwango ambacho nilijisababishia matatizo makubwa katika
familia yangu na kazini, lakini sijawahi kutetereka na sijaterereka. Nilifanya
yote haya kwa mapenzi yangu ya dhati na imani yangu kwa CHADEMA kwamba ndicho
chama kinachostahili kuongoza harakati za mabadiliko hapa nchini kwa sasa.
c.
Nasikitika kwamba nimesababisha
usumbufu kwa viongozi wangu wa CHADEMA kutokana na dhamira yangu ya kutaka
mabadiliko ya uongozi ndani ya chama chetu kwa njia halali za kidemokrasia.
Nilifanya hivi kwa imani niliyo nayo kwa misingi ambayo CHADEMA inasimamia,
ikiwemo demokrasia, na imani yangu kwamba chama hiki kinahitaji kufanya
mabadiliko makubwa katika uongozi wa juu wa chama, ikiwa ni maandalizi muhimu
kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Nasisitiza tena kwamba siamini hata
kidogo kwamba matamanio ya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama, na kuandaa
mikakati ya kufikia matamanio hayo kwa njia za kidemokrasia ni uhaini.
d.
Tunaweza kujifunza kutokana na
historia. Siasa za ushindani ndani ya vyama katika nchi hii sio kitu kigeni. Enzi
za TAA na kabla TANU haijazaliwa wanachama walikuwa wanagawana nafasi za
uongozi mezani. Lakini mwaka TANU ilipozaliwa (mwaka 1954) kulikuwa na uchaguzi
mkali sana kwa nafasi ya uenyekiti. Mwalimu Nyerere alimshinda Mzee Skyes kwa
kura chache sana. Rais Obama wa Marekani alianza mkakati wa kushinda uteuzi wa
kugombea nafasi ya urais kupitia chama chake cha Democrat mapema kabisa mwaka
2006 kupitia waraka maalumu wa siri
ulioainisha mikakati yake. Waraka huu uliandaliwa na watu
wanne tu bila yeye mwenyewe kujua. Waandaji wa mkakati huu walikuja
kumshirikisha baadaye mwaka 2007 na kumshawishi yeye ajitokeze kugombea
dhidi ya Hillary Clinton aliyekuwa anachukuliwa kama mrithi halali wa kiti cha
urais. Yaliyobaki ni historia. Hivi ndivyo ambavyo siasa za ushindani ndani ya
vyama hatimaye huzaa wagombea na viongozi imara katika nchi.
e.
Zitto Zuberi Kabwe hajafukuzwa kwa
sababu ya waraka huu kwa sababu yeye hakuhusika kwa namna yeyote kuandaa,
ingawa alikuwa ni mlengwa mkuu. Yeye amefukuzwa kwa sababu ambazo yeye
atazieleza na ambazo viongozi wa CHADEMA hawakuzieleza katika mkutano na
waandishi wa habari.
f.
Napenda ijulikane kwamba sikuomba
kujiuzulu kwa sababu ya kuogopa aibu ya kufukuzwa. Niliomba kujiuzulu kwa
sababu nilitambua kwamba wenzangu katika Kamati Kuu walikuwa hawana imani nami
tena, na ni uungwana kujiuzulu mkifika mahala hamuaminiani. Nilitambua vilevile
kwamba, kwa mujibu wa Katiba yetu, Kamati Kuu ilikuwa haina uwezo wa kunivua
nafasi yangu moja kwa moja. Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, Sura ya Sita,
Ibara ya 6.3.6 (b), inasomeka hivi “Kiongozi aliyeteuliwa na vikao vya uongozi
ataweza kusimamishwa au kuachishwa uongozi na kikao kilichomteua”. Mimi
nilichaguliwa na Baraza Kuu na ni kikao hiki pekee chenye uwezo wa kunivua
nafasi niliyokuwa nayo. Ninaamini wajumbe wa Kamati Kuu walipitiwa katika
hili kwa sababu siamini kwamba hawajui takwa hili la kikatiba ukizingatia
kwamba ndani yake kuna wajumbe waliobobea kabisa katika tasnia ya sheria.
4.
Hiki kilichotokea ndani ya chama sio
kitu kibaya. Vyama vingi imara hupitia katika migogoro na misukosuko kama hii
na zaidi. Naamini tutavuka na tutakuwa imara zaidi. Muhimu ni kwamba ni lazima
tuaminiane. Katika kuaminiana sio lazima tufanane kimawazo na kimtazamo kwa
sababu hili ni jambo lisilowezekana kibinadamu na zaidi katika siasa
5.
Ninapohitimisha, ninawasihi
wanachama wa CHADEMA na wapenzi wa mabadiliko popote walipo wapiganie kwa dhati
MISINGI mama ya CHADEMA ikiwemo demokrasia ndani ya chama. Hakuna namna ambavyo
chama chochote kinaweza kushawishi umma kwamba kitapigania demokrasia katika
nchi wakati kinayahainisha mapambano ya kidemokrasia ndani ya chama chenyewe.
Kukataa siasa za ushindani ndani ya chama ni kuhujumu
demokrasia na ni usaliti kw misingi mama ya chama ambayo ni uhuru wa kweli na
mabadiliko ya kweli. Hisia za usaliti na umamluki zilitumika enzi za
ukomunisti katika kunyamazisha wapinzani ndani ya vyama vya siasa na katika
nchi. Zilikuwa ni njia haramu zilizozoeleka ambazo hatimaye zilizaa udikteta wa
kutisha katika mataifa ya kikomunisti. Tusikubali utamaduni wa kuhisiana
usaliti na umamluki ukaota mizizi katika chama chetu na katika nchi kwa sababu
utaua demokrasia na mfumo wa vyama vingi utakuwa hauna maana tena.
6.
Nitafuata taratibu zote za chama
kama zilivyoelekezwa na Kamati Kuu na kwa mujibu wa katiba yetu, na nitashiriki
kikamilifu katika kutuliza hali ya kisiasa ndani ya chama ili kuhakikisha
kwamba tunabaki imara, na CHADEMA inaendelea kuwa tumaini la watanzania.
Mungu ibariki Tanzania.
Dkt. Kitila Mkumbo
Dar es Salaam