m

"If you want to conquer fear, don't sit at home and think about it. Go out and get busy. "

-- Dale Carnegie, motivational expert

Tuesday, 9 April 2013

Uhuru Kenyata aapishwa kuwa rais wa nne wa Kenya

Viongozi kutoka mataifa kadhaa ya Afrika wamewasili jijini Nairobi kuungana na Wakenya kwenye sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kwenye uwanja wa mpira uliojaa maelfu ya wafuasi wake.
Kenyatta mwenye umri wa miaka 51 ni mtoto wa rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta. Ushindi wake wa asilimia 50.07 katika uchaguzi wa tarehe 4 Machi ulihalalishwa na Mahakama ya Juu baada ya pingamizi lililowekwa na Waziri Mkuu anayemaliza muda wake, Raila Odinga, kutupiliwa mbali na mahakama hiyo.
Kenyatta anayekuwa rais wa nne wa taifa hilo la Afrika ya Mashariki tangu lilipopata uhuru wake kutoka Uingereza mwaka 1963, anakuwa rais wa pili barani Afrika kuwa madarakani hali anakabiliwa na mashitaka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa tuhuma za kusaidia kuchochea ghasia za kikabila zilizoukumba uchaguzi wa urais wa Kenya wa mwaka 2007. Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mwezi Julai, ambapo Kenyatta na naibu wake, William Ruto, wanakabiliwa na mashitaka ya aina moja.
Hata hivyo, uchaguzi wa mara hii ulikuwa wa amani na kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Wakenya wengi wanatarajia kwamba Uhuru atatimiza ahadi yake ya kuwa kiongozi wa watu wote na hatakuwa rais wa kabila lake tu, jambo ambalo limekuwa kawaida kwa wanasiasa wa huko.
Utata unaoyakumba mataifa ya Magharibi
Kenya's President Uhuru Kenyatta (C) displays the special Rais Uhuru Kenyatta akikabidhiwa upanga wa mamlaka na rais wa zamani Mwai Kibaki Rais Uhuru Kenyatta akikabidhiwa upanga wa mamlaka na rais wa zamani Mwai Kibaki
Kwa mataifa ya Magharibi, ambao ni wafadhili wakubwa wa nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi kwenye eneo la la mashariki mwa Afrika, Kenya ni mshirika muhimu katika mapambano dhidi ya makundi ya kidini yenye siasa kali kwenye eneo hilo.
Lakini sasa mataifa hayo yanakabiliwa na uchaguzi wa ama kuendelea kuimarisha mahusiano au kujitenga na kiongozi ambaye anakabiliwa na mashitaka kwenye mahakama ya ICC mjini The Hague.
Marekani na mataifa makubwa ya Ulaya yalisema yangelituma mabalozi wao kwenye sherehe za kuapishwa kwa Kenyatta, kiwango cha uwakilishi ambacho wanasema bado kinakwenda sambamba na msimamo wao wa kuwa na mahusiano ya lazima tu na watuhumiwa hao.
Mtaalamu wa masuala ya Kenya katika Chuo Kikuu cha Warwick, Daniel Branch, ameiambia Reuters kuwa mataifa ya Magharibi yamejikuta kwenye hali ngumu sana, lakini huenda kila nchi ikatafuta njia yake yenyewe na mahusiano na Kenya.
China huenda ikapata fursa mpya
Wanajeshi wa Kenya wakati wa kuapishwa Uhuru Kenyatta. Wanajeshi wa Kenya wakati wa kuapishwa Uhuru Kenyatta.
Ikiwa mataifa ya Magharibi yatagawika kuhusu mahusiano yake na Kenya chini ya Uhuru Kenyatta, hali hiyo itafungua njia zaidi kwa China na mataifa mengine makubwa ya Asia ambayo yamekuwa yakijizolea ushawishi wa kisiasa na kibiashara barani Afrika kwa siku za hivi karibuni.
Wakati kwenye sherehe hizo, viongozi wakuu wa Afrika watajikuta wamewekwa pamoja na mabalozi tu wa nchi za Magharibi, Kenya na India - ambazo zote mbili hazijasaini Mkataba wa Rome ulioanzisha ICC - zimetuma maafisa wao wa ngazi za juu.
Hata hivyo, mabalozi wa Kimagharibi wataepuka matusi mengine, baada ya maafisa wa Kenya kusema kuwa Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan asingelihudhuria sherehe hiyo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Josephat Charo

DW.DE

Serikali yarudisha viboko shuleni

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo 


Posted  Jumatatu,Aprili8  2013  saa 21:1 PM
Kwa ufupi
Kadhalika alisema Serikali imepiga marufuku matumizi ya simu za mikononi kwa sababu baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakizitumia vibaya jambo ambalo linawarudisha nyuma kimasomo. 

Mpoki Bukuku, MWananchi
Serikali imesema itarudisha adhabu ya viboko kwa wanafunzi shuleni ili kujenga nidhamu na kujituma.Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akizindua tovuti ya www.shledirect.co.tz inayowezesha wanafunzi kujisomea kwa njia ya mtandao, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo ilisema kuondolewa kwa adhabu ya viboko shuleni kumewafanya wanafunzi wengi kukosa nidhamu na wakati mwingine kujifanyia mambo kienyeji.

“Wasipotandikwa mambo hayaendi, nilipokuwa mwalimu mkuu nilikuwa nawatandika kweli ndiyo maana shule yangu ilikuwa ikiongoza Mkoa wa Mbeya hivihivi hawaendi...” alisema huku akishangiliwa na wageni waalikwa.

Alisema watoto wa siku hizi wamekuwa wakitumia vibaya teknolojia ambayo ingeweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika masomo yao... “Tovuti kama hiyo ingewasaidia kwa masomo, lakini wao wanakimbilia kwenye facebook na mambo mengine yasiyofaa.”

Aliyalaumu mashirika yasiyo ya kiserikali na haki za binadamu ambayo yamekuwa yakipigania kuondolewa kwa adhabu hiyo shuleni na kusababisha kushuka kwa nidhamu kwa kiasi kikubwa.

Kadhalika alisema Serikali imepiga marufuku matumizi ya simu za mikononi kwa sababu baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakizitumia vibaya jambo ambalo linawarudisha nyuma kimasomo.
“Simu tunazipiga marufuku, mwalimu akimkuta mwanafunzi na simu amnyang’anye ndizo zinatuharibia taifa letu.”

Aliwapongeza wabunifu wa mtandao huo akisema ni wazalendo kwani wamekuwa msaada katika jitihada za Serikali kukuza elimu nchini.

“Watu wanapiga kelele Mulugo na Kawambwa wajiuzulu, hata tukijiuzulu haitasaidia, bali kila Mtanzania atoe mchango wake katika elimu ili kuweza kuiendeleza.”
Mwanzilishi wa tovuti hiyo, Faraja Nyalandu alisema itakuwa na manufaa kwa wanafunzi wa Tanzania kwani masomo yanayotolewa yanaandaliwa na walimu wazoefu wenye shahada hivyo wanafunzi watakapoitumia watapata manufaa makubwa.

Maoni ya wadau
Akizungumzia hatua hiyo ya Serikali, Waziri Kivuli wa Elimu Mafunzo ya Ufundi, Suzan Lyimo aliitaka iache kuangalia mambo madogo ambayo yanachangia kwa kiasi kidogo tu kudorora kwa elimu na kuacha mambo makubwa.

“Kuna mambo makubwa zaidi yaliyotufikisha hapa tulipo, hii ni sawa na kushughulika na matawi na kuacha mizizi. Lazima tuangalie suala hili kwa upana zaidi, kuna ripoti nyingi na nzito hazijafanyiwa kazi mpaka sasa badala yake Serikali inaibuka na kuanza kutangaza vitu vidogo kama hivyo, wafanyie kazi kwanza ripoti ambazo zilitumia pesa nyingi za walipakodi kwani nyingi zina mapendekezo mazuri.”

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mpwapwa, Rukonge Mwero alisema uzuri wa adhabu ya viboko ni kwamba haipotezi muda”

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo Bisimba alisema adhabu ya viboko haina maana katika kipindi hiki akisema wanafunzi wanapaswa kupewa adhabu ambazo zinawafundisha kama zile za kufanya usafi na kazi mbalimbali.

“Viboko havifundishi zaidi ya kumpatia mwanafunzi maumivu na kusababisha aichukie shule. Waelimishwe kwa kuelekezwa lakini wakiendelea kukiuka, wapewe adhabu za kufanya kazi mbalimbali.

Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alisema walimu hawapati faida yoyote kuwachapa au kutowachapa viboko wanafunzi.“Hawa viongozi kila kukicha wanazungumza mambo yasiyo na maana, badala ya kuzungumzia masilahi ya walimu wanazungumza kuhusu viboko, hatuelewi wakiamka kesho watasema nini,” alisema Mukoba.
Chanzo; Mwananchi.co.tz