m

"If you want to conquer fear, don't sit at home and think about it. Go out and get busy. "

-- Dale Carnegie, motivational expert

Friday, 10 January 2014

Mpango kwa Vijana na Mustakabali wa Ajira



Wapenzi wangu leo nipo tena ili kukushirikisha katika habari zetu KII. Kama ujuavyo moto wetu ni “habari ni Maisha” kumbe ukikosa habari huna maisha na ukipata habari njema utakuwa na maisha mema na ukipata habari mbaya ni matokeo ya maisha mabaya. Kilichopo mezani leo ni juu ya vijana wenzangu na mpango unaopaswa kuwasaidia vijana.
Ndugu zangu sina mpango wowote unaoweza kuwasaidia vijana lakini nafikiri kwamba ni stahiki sana kuwa na mpango huo kama tunalitakia mema Taifa letu. Kumekuwa na ongezeko la vijana nchini, katika ongezeko hilo kuna kundi kubwa la vijana wasio na elimu wala ajira na kundi la pili ni lile lililo katika mfumo wa elimu na hata kupata elimu lakini likiwa na wasiwasi wa ajira. Ongezeko hilo ndio linalonitia wasiwasi na hatima ya Taifa letu hivyo kunisukuma kuandika makala haya.
Kabla sijaendelea naomba nigusie uhalifu katika majiji makubwa na yanayoongoza kwa uhalifu duniani, nazungumzia Paris –ufaransa Rio De Jeneiro- Brazil na Johannesburg- Afrika kusini. Ndio majiji hatari zaidi duniani kwa uhalifu lakini swali la kujiuliza ni nani wanaofanya uhalifu huo? Na kwanini? Kwa haraka utagundua kuwa majiji hayo ndio yale yenye vijana wengi waliokosa ajira. Katika majiji hayo matatu utabaini zaidi kuwa majiji mawili ni yale yenye mgogoro wa ubaguzi wa rangi. Sitaki kuzungumzia sana ubaguzi wa rangi bali nataka kugusia ubaguzi na mipango mibovu kwa vijana katika maendeleo ya Taifa lolote duniani Tanzania ikiwa mfano. Afrika kusini ilikumbwa na ubaguzi wa rangi na katika ubaguzi huo uligusa pia elimu na ajira pasipo kujali athari itakayopata baadaye. Hali kadhalika Paris ilikumbwa na wahamiaji haramu wa Afrika kaskazini hasa kutoka nchi za Algeria na makoloni yake kama Senegal. Wahamiaji wakaingia  nchini ufaransa na wenyewe wakawaadhibu si tu kuwafukuza bali hata waliobaki kwa kuwabagua kama wasio na haki nchini humo. Athari yake ndio yanayowapata sasa kwani wale vijana waliobaguliwa na kunyimwa elimu au ajira sasa wamegeuka kuwa wahalifu kama njia yao ya kujikimu na maisha.
Unapoamua kuwa mbaguzi lazima ujitenge kabisa jamii ile unayoibagua na ikiwa umeamua kuishi nayo ni lazima ukatae ubaguzi kwa gharama zote, huwezi kumbagua siku zote mtu unayeishi naye mahali pamoja.
Nchi yetu sasa ina ongezeko kubwa la vijana wasomi na wasio wasomi bila kuwepo na mipango madhubuti  ya kuwasaidia kukabili changamoto ya ajira. Watawala hujisahau sana kuhusu vijana kwani huona wao na familia zao wako salama hakuna tatizo lolote kwani hata ajira zimekuwa kwa kibendera. Hakuna mipango  ya makusudi ya kuwasaidia vijana katika ajira na ukizingatia mfumo wetu wa elimu unamuandaa kijana kuwa afisa wa kukaa ofisini tu, mfumo wa elimu ya kikoloni ili wakoloni kujipatia maofisa wachache katika ofisi zao kuendelea kuwatawala waafrika. Kuna haja ya kuwepo kwa mipango ya namna vijana wanavyoweza kutengeneza ajira mbali ya kung’ang’ania zile za serikali na mashirika kwani tayari kuna wasomi wengi kwa ngazi ya sekondari, astashahada, stashahada hadi shahada wasio na ajira na bado wana matumaini ya kuajiriwa. Wana matumaini makubwa kila watazamapo vyeti vyao lakini ukweli ni kwamba hakuna ajira nchi hii tupilia mbali zile chache ziwatoshao wenyewe. Nchi isiyo na viwanda, isiyo na miundombinu ya afya na elimu haiwezi kuwa na ajira za kutosha kwani wataalamu ambao wangeajiriwa kwenye hospitali, shule, vyuo, migodini na viwandani itawalazimu kubaki wakirandaranda mitaaani wakiwa na matumaini ya ajira ilhali hakuna ajira.
Mpango niutakao ni kuwabadili vijana wasifikiri juu ya njia moja ya ajira yaani kutegemea kuajiriwa badala yake kujiaajiri, wafunzwe kwamba ajira ni pamoja na kujiajiri  na hata kutengeneza ajira kwa ajira kwa ajiri ya wengine. Serikali inapaswa kufanya mambo mawili muhimu kubadili mtazamo wa vijana katika ajira na pili ni kuwasafishia njia ya kujiajiri. Binafsi sioni njia bora ya kujiajiri katika nchi zaidi ya viwanda na kilimo ndio nafasi zinazopaswa kupewa kipaumbele. Nchi ya Tanzania bado haijawa ya kiviwanda na wala sioni kama ni nchi ya kilimo inababaika tu lakini tunaweza kuleta mageuzi na mageuzi yoyote huletwa na vijana hata uhuru wa Afrika uliletwa na vijana machachari akina Kwame Nkrumah, Mwl. J.K Nyerere, komredi R. Mugabe na wengineo. Tugeukie viwanda kwani nchi yetu ina matumizi makubwa kabisa ya bidhaa za viwandani lakini ajabu ni kwamba asilimia kubwa ya bidhaa hutoka nje ya nchi. Kama ni elimu tayari tunayo japo viwanda vingine havihitaji elimu, kwani ni elimu gani inahitajika ili kutengeneza vijiti vya meno (Toothstick), Kalamu, rula, chaki n.k mbona navyo vyatoka nje? Ni dhahiri kuwa kama vingetengenezwa nchini tungetengeneza ajira kwa vijana wengi kabisa. Inashangaza kuona nchi bado inategemea bidhaa ndogondogo za nyumbani kama sabuni, sukari, chumvi, kutoka nje ya nchi na watanzania wakiona fahari kutumia bidhaa za nje kuliko za ndani. Binafsi nimekuwa nikitoa semina za ujasiriamali ninapopata nafasi ya kufanya hivyo katika pitapita yangu katika mitandao ni mebaini kuna mitambo ya hadi milioni 8 na hata ya chini ya hapo inayoweza kuchonga bidhaa ndogondogo kama mishumaa, vijiti vya meno na kutengeneza chaki ni mitambo rahisi isiyohitaji elimu kubwa. Mbali ya hivyo serikali iliyoweza kuwashawishi wenye viwanda kutoka nje kama kiwanda cha Nation kilichokuwa kinazalisha betri na redio za nation inashindwaje leo kuwashawishi Wajapan, wachina na wahindi kuleta viwanda vyao nchini ili tusiendelee kuagiza bidhaa za kielekroniki kama redio, ngamizi, simu na magari wakati sisi ni wateja wao wakubwa? Sijui wizara inayohusika na viwanda inafanya nini kuhusu hili na wizara inayohusika na ajira inaishauri nini wizara ya viwanda? Kama hakutakuwa na hatua za makusudi kuongeza viwanda vidogo na vya kati ajira itaendelea kuwa tatizo kubwa na mfumuko wa bei utakuwa donda ndugu katika nchi yetu kwani tumekuwa na matumizi makubwa ya fedha za kigeni kuliko uzalishaji.
Katika kilimo bado hatujaamua kukifanya kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu na hatimaye kutengeneza ajira. Kwetu kilimo imebakia kuwa sekta ya walalahoi na watu waliokosa elimu, fikra potofu kabisa. Hebu tazama pamoja na kuwepo kwa mapori mengi bado nchi imekuwa na tatizo kubwa la chakula katika mikoa ya Shinyanga, Singida na Dodoma. Maana yake mahitaji ya chakula yamekuwa makubwa kuliko uzalishaji wakati huohuo kukiwa na tatizo la ajira. Watu hawana la kufanya wakati mapori yanakaa bure na mahitaji ya chakula ni makubwa. Ni ajira ngapi tupata kama tukamua kuzalisha chakula cha kutosheleza mahitaji yetu potelea mbali kuzalisha kwa ajili ya kuuza nje ya nchi ambako pia kuna mahitaji makubwa ya chakula? Ajabu zaidi hata matunda yanatoka Afrika ya Kusini kwa mfano Tufaha maarufu kama apple huagizwa kutoka Afrika ya kusini ingawa yanastawi maeneo ya baridi kama Iringa na Njombe. Kuna haja gani ya kunywa maziwa ya Kenya ili hali tuna mamilioni ya ng’ombe nchini? Nina maswali mengi yakisubiri majibu.

China tuionayo leo hatukuwa na tofauti sana tulipokuwa tunapata uhuru,  imestawi sana baada kujihakikishia kwanza soko la ndani la bidhaa zake yaani wananchi wake yenyewe, wakafanya uzalishalishaji mkubwa ndipo kutanua uchumi wake na kuweza kushindana na mataifa makubwa kiuchumi. Nasi tuna soko letu la ndani kwani watu milioni arobaini na uchee si haba. Tukizalisha kwa ajili yetu tu tutaiimarisha shilingi yetu na hatimaye kuwa na uchumi unaostawi lakini vijana wakipata utulivu kwa ajira kemkem.

Tazama utengenezaji wa vijiti vya meno
 Picha za mashine rahisi za kutengeneza vijiti na mishumaa


Lazima uandaliwe mpango kwa ajili ya vijana na kupata mustakabali wa  baadaye wa kwao wenyewe vijana na Taifa letu. Kama haitafanyika hivyo nchi hii haiitakuwa salama tena kwani wasionacho watapopoteza matumaini utakuwa mwanzo wa uhalifu mkubwa kwa walionacho. Hatuna tofauti na nchi za Ufaransa na Afrika Kusini kwani hata elimu yetu ni ya kibaguzi kwa sehemu kwani  wenye nacho wanapata elimu bora kuliko wasionacho na katika ajira vivyo hivyo.
Hata hivyo ninatoa rai kwa vijana kuwa tayari kwa ajili ya ajira yoyote yenye kuingiza kipato wawe tayari kutumia uwezo wao wote kubuni ajira ili kuleta mageuzi kama tukitaka ajira za serikali tu nchi yetu itaangamia na katika kuangamia huko athari kubwa ni kwa makabwela kama siye.
Wako katika safari                                                   
Ndg. Peter Kapagi                                                                                                    09.01.2014
                                                                                                                                    Mbeya

Uganda,Rwanda, Kenya wakubaliana himaya moja ya ulinzi

Mawaziri wa ulinzi na wa mambo ya ndani kutoka nchi za Uganda,Rwanda na Kenya wametia saini makubaliano kuweka himaya moja ya ulinzi miongoni mwa nchi hizo.
Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki-kutoka kushoto: Uhuru Kenyatta, Yoweri Museveni na Paul Kagame Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki-kutoka kushoto: Uhuru Kenyatta, Yoweri Museveni na Paul Kagame
Hii ni mara ya kwanza kuwepo kwa mkataba huo na hii ina maana nchi moja ikipata matatizo ya usalama nchi nyingine zitakuwa na uhuru wa kuingilia kati na kusaidia. Kikao cha mawaziri hao kilitanguliwa na kile cha wakuu wa majeshi na polisi kutoka nchi hizo ambacho pia kilitathmini changamoto za kiusalama kwenye eneo hilo na jinsi ya kuimarisha ushirikiano miongoni mwa mataifa hayo. Kutoka Kigali mwandishi wetu Sylivanus Karemera anaripoti zaidi. Kusikiliza ripoti hiyo bonyeza alama ya spika za masikioni hapo chini.
Mwandishi: Sylivanus Karemera
Mhariri: Mohammed Khelef
chanzo:dw.de

Wamarekani wapambana na baridi kali kuwahi kutokea.


  • Mwanamke anatembea katika hali ya baridi kali mjini Chicago, Illinois, Jan. 6, 2014.
    Wakazi wa mashariki na kusini mwa Marekani wanapambana na baridi kali na ya hatari kuwahi kutokea baada ya dharuba ya upepo baridi kutoka maeneo ya kaskazini ya bara la Amerika kupiga na kuenea maeneo ya kati, kusini na mashariki ya nchi hii.
    Hali ya baridi inayoweza kugandisha maji kuwa barafu na theluji katika muda wa sekunde chache imevunja rekodi ya baridi iliyotokea miaka 10 iliyopita na kufanya hali kuwa hatari kubaki nje na kusababisha maelfu ya shule na biashara kufungwa.
    Kiwango cha baridi kimeshuka chini kwa nyuzi 10 chini ya sifuri kwenye kipimo cha Celsius hapa Washington DC , Philadelphia na Boston huku upepo ukiwa ni baridi zaidi na kufanya mtu kuhisi baridi kuwa chini ya kipmo hicho.
    Wakazi wa Marekani wazungumzia baridi kali.

    Kushuka sana kwa kiwango cha baridi kumesababisha kuahirishwa kwa maelfu ya safari za ndege na kuleta mtafaruku barabarani na kwenye njia za reli. Watabiri wa hali ya hewa wanasema karibu watu milioni 200 wanaweza kuathiriwa na hali hiyo.

    Baadhi ya wahamiaji kutoka Afrika Mashariki wanasema hali hii inawasababisha kukumbuka nyumbani na hawajawahi kuona kitu kama hichi ambapo usipojitahadhari unaweza kuwa mgonjwa mara moja au hata kupoteza vidole vya mikono au miguu ikiwa hujavaa vizuri.

    Hali hii ya baridi pia inafikia maeneo ya kusini ambayo ni nadra kupata baridi kama vile Florida na kusini mwa Texas kawaida maeneo hayo huwa wanapata baridi ya wastani  tu wakati huu wa majira ya baridi.
    Maafisa wameamua kufunga mashule ili watoto wabaki salama kutokana na baridi kali, ambayo inaweza kupelekea vidole kukatika katika dakika chache kama ngozi ikiachwa wazi. 
    Chanzo: voaswahili.com