
Kisima kilichopo eneo la Matamwe Mkoa wa Kaskazini Unguja ambamo raia
wawili wa Ufaransa wanasadikiwa kuuawa na kisha kufukiwa kwa zege. Picha
na Mwinyi Sadallah
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Posted Februari1 2014 saa 9:33 AM
Posted Februari1 2014 saa 9:33 AM
Kwa ufupi
- Maiti zao zaingizwa kwenye kisima cha maji na kufunikwa kwa zege, watatu washikiliwa kwa tuhuma za kushiriki mauaji hayo
Zanzibar.Raia wawili wa
Ufaransa wameuawa na kutumbukizwa katika kisima cha maji kilichomo ndani
ya uwanja wa nyumba yao na watu wasiojulikana katika eneo la Shehia ya
Matemwe Kaskazini, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Yussuf Ilembo zinaeleza
kuwa watu hao mtu na mkewe waliuawa hivi karibuni.
DCI Ilembo aliliambia gazeti hili jana kuwa tayari
vikosi vya Zimamoto na Uokozi (KZU) na Polisi vimeanza kufukua kisima
hicho na kwamba katika hatua ya awali wamefanikiwa kukuta mfupa wa mguu
wa kushoto wa mmoja wa watu hao.
Aliwataja wazungu hao kutoka Ufaransa kuwa ni
Francois Cherer Robert Daniel na Brigette Mary ambao walikuwa wakiishi
kama mtu na mkewe wakiwa na mbwa wao anayeitwa Allan ambaye pia amekutwa
amekufa ndani ya nyumba hiyo.
Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa
Wafaransa hao waliingia nchini kihalali mwaka 2013, na kununua nyumba
kwenye ufukwe wa mwambao wa Bahari ya Hindi eneo la Matemwe na kuanza
kuishi eneo hilo.
DCI Ilembo alisema polisi tayari wanawashikilia
watu watatu wakazi wa Shangani katika Mjimkongwe wa Zanzibar na mmoja
anayeishi katika eneo la Kilimani katika wilaya ya Mjini Unguja.
“Kuna askari wanaendelea na kazi ya kuzamia ndani
ya kisima kilichomo ndani ya uzio wa nyumba hiyo, kazi bado ni kubwa na
siyo ya siku moja,” alisema DCI Ilembo.
Gazeti hili limefanikiwa kufika katika eneo la
nyumba hiyo na kukuta askari Polisi wanne wakilinda nyumba hiyo huku
harufu kali ikitoka katika shimo la kisima.
Hata hivyo, mlinzi wa nyumba hiyo ametoweka katika mazingira ya kutatanisha na simu yake kila ikipigwa imezimwa.
Mlinzi mpya aitwaye Omar Juma ambaye amekutwa
akilinda nyumba hiyo baada ya kuajiriwa na mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa
amesema alikabidhiwa kazi ya ulinzi kuanzia Januari mwaka huu na
hakumkuta mtu yeyote akiishi hapo.
“Kazi yangu ni kazi za ulinzi, nimeletwa hapa na
mwajiri, sijui lolote, mwajiri wangu ndiye anayejua kama kulikuwa na
watu kabla au la, sina la kusema na sijui nianzie wapi,” alisema Omar.
Soma zaidi http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Wafaransa-wawili-wauawa-Z-bar/-/1597296/2168588/-/ns6sne/-/index.html
Soma zaidi http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Wafaransa-wawili-wauawa-Z-bar/-/1597296/2168588/-/ns6sne/-/index.html