Bwana Harusi Fadhili Mahenge akiwa ndani ya Suti akisubiri kufungishwa ndoa |
Bi Harusi Naomi Ngoje akiwa amejilalia chumbani akisubiri hatima ya Wazazi ndipo ajiandae kwenda kanisani tayari kwa kufunga ndoa na mchumba wake waliodumu kwa miezi saba. |
Bwana harusi akiwa na mpambe wake kanisani wakimsubiri bibi Harusi |
Askofu Kenani Mpalala akiwa katika picha ya pomaja na Bwana Harusi na mpambe wake muda mfupi baada ya kuwasili kanisani |
Askofu Keenan Mpalala wa kanisa la Free Pentecost Church of Tanzania akionesha tangazo la Ndoa |
Baadhi ya ndugu wa mwanamke wakiwa katika kikao na kuendelea na msimamo wao kuwa mahali lazima imalize ndipo wamtoe binti yao |
Jamaa wameshika vichwa hali haieleweki |
Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilolo Ndugu Benson Mbwana(aliyevalia shati rangi ya Zambarau) akionyesha ratiba ya sherehe. |
Baadhi ya akina mama wakiangalia ratiba ya harusi |
Kanisani |
Baadhi ya waumini na majirani wakisubiri kanisani |
KATIKA
hali isiyokuwa ya kawaida Familia moja ya Makunguru Mtaa wa Ilolo
Jijini Mbeya imesababisha sintofahamu dhidi ya Familia nyingine baada ya
kumkatalia binti yao kuolewa kwa madai ya waoaji kutokamilisha Mahari
waliyokuwa wamepangiwa.
Tukio
hilo la aina yake limetokea leo ambapo Bwana harusi aliyefahamika kwa
jina la Fadhili Mahenge(28) Mkazi wa Songea aliyekuwa amuoe Naomi Ngoje
na harusi yao kufungwa katika kanisa la Free Pentecoste Church Of
Tanzania(FPCT) lililopo Makunguru Jijini hapa kushindwa kufungwa baada
ya wazazi wa Bibi harusi kuzuia ndoa hiyo hadi Mahari itakapokamilika.
Wakizungumzia
tukio hilo Nyumbani kwa Familia ya Bibi Harusi, Mjomba wa Bibi Harusi
Dickson Ngoje amesema tatizo la wao kugomea ndoa hiyo ni kutaka waoaji
kutimiza masharti waliokuwa wamekubaliana awali ambayo hadi siku ya
mwisho familia hiyo haijatekeleza.
Amesema
siku ya kwanza waoaji walifika Nyumbani kwa Mzee Ngoje na
kujitambulisha ambapo walipangiwa taratibu za mahari kwa mujibu wa Mila
kuwa watatakiwa kutoa Blanket 2, Mashuka mawili, Mkaja(200,000), mbuzi
4, Majembe 4, Ng’ombe Jike 2 na Ngo’mbe Dume 1 pamoja na fedha taslimu
Shilingi Laki 3.
Amesema
baada ya Familia hiyo ya Waoaji ambao ni Ukoo wa Mahenge kupangiwa vitu
hivyo waliondoka na kuahidi kurudi siku nyingine kwa ajili kukamilisha
vitu walivyopangiwa ambapo walirudi Septemba 11, Mwaka huu wakiongozwa
na Mshenga aliyejulikana kwa jina moja la Mzee Katete wakiwa na Blanketi
2, Mashuka mawili pamoja na Fedha shilingi 10,000/= ambazo walizipokea
na kuwaambia hawawezi kuzungumza chochote juu ya Ndoa.
Mjomba
huyo anaongeza kuwa baada ya wiki mbili familia hiyo ilirudi na kukuta
Nyumbani kuna ukoo mzima wakiwa na Shilingi 200,000/= ndipo walipoambiwa
walipe kiingilio shilingi 100,000/= ndiyo wanaweza kupokelewa nyumbani
jambo ambalo walilitekeleza kisha kulipa fedha walizokuwa nazo kama
Mkaja na kuomba wapewe kibali cha kuandikisha ndoa na taratibu za
kumalizia vilivyobaki zikiendelea.
Anasema
tangu hapo Ndoa ilianza kutangazwa Disemba 8 na kuisha Disemba 22,
Mwaka huu baada ya kutangazwa mara tatu huku tangazo likiashiria ndoa
kufungwa tarehe 28/12/2013 ambapo wazazi wakiahidi kumalizia Mahari
iliyobaki kabla ya siku ya kufunga ndoa.
Akizungumzia
kwa kirefu kashishe hiyo, Mjomba huyo anasema baada ya wazazi wa
Mwanaume kusisitiza kumaliza kila kitu hadi ifikapo Disemba 23, Mwaka
huu na wao walijikusanya na kupanga taratibu za sherehe hususani ya
kumwaga binti yao(Send Off) ambayo ilifanyika Disemba 24, Mwaka huu.
Aidha
baadhi ya ndugu wameongeza kuwa familia hiyo haioneshi uaminifu wa
kumalizia Mahari hiyo kutokana na ahadi zisizotekelezeka walizotoa tangu
kipindi cha nyuma na kuongeza kuwa hata kwenye sherehe ya kumwaga binti
yao walifika baadhi ya ndugu wakiwa na Zawadi tofauti na taratibu
zinavyotaka.
Wamesema
kwa mujibu wa taratibu za Sherehe za SendOff upande wa Mwanaume
unatakiwa kuleta zawadi ambazo ni nguo za Bibi Harusi za kuvaa siku ya
Ndoa Pamoja n Harusi lakini wao hawakufanya hivyo ingawa walikuwa na
Nguo ambazo tayari zilikuwa zimetumika.
Kwa
upande wa Mchungaji aliyekuwa anataka kufingisha Ndoa hiyo ambaye pia
ni Askofu wa Kanisa hilo, Mchungaji Kenan Mpalala alipoulizwa kuhusu
hali hiyo amesema kwa mujibu wa taratibu za Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971
kifungu cha 8 pingamizi litolewe ndani ya siku 21.
Amesema
upande wa Wazazi wa Mwanamke ulishindwa kuwasilisha pingamizi lao
kanisani kabla ya Siku 21 badala yake walifika kutoa malalamiko kuhusu
kutomaliziwa kwa mahali jambo ambalo alisema yeye kama Mwandikisha Ndoa
halimhusu bali pande mbili wanatakiwa kulimaliza kabla ya Ndoa.
Naye
Bwana Harusi Mtarajiwa Fadhili Mahenge(28) alipoulizwa kuhusiana na
suala hilo huku akiwa tayari Kanisani kwa ajili ya Kufungishwa Ndoa
alisema anachosubiri ni hatma ya Wazazi wa Mwanamke kama wanaweza
kumwachia Mkewe iliwanachodai awe anamalizia taratibu.
Amesema
yeye kama yeye kwa sasa hana fedha zozote za kuweza kumalizia
anachodaiwa zaidi ya kuomba busara za wazazi wa Mwanamke kumruhusu Ndoa
ifungwe ndipo aweze kulipa Mahari anayodaiwa kwa awamu kutokana na hali
yake ya kiuchumi kuwa Mbaya.
Ameenda
mbali zaidi kwa kusema kama Wazazi wa Mwanamke wataendelea kuwa na
Msimamo huo basi hata yeye ataomba arudishiwe kile alichokitoa awali ili
ajipange upya kwa ajili ya ndoa baada ya kukamilisha madai yao.
Hadi
tunaingia mtamboni Mbeyayetu ambayo ilikuwepo sehemu ya tukio timu ya
usuluhishi ilikuwa ikiendelea na kazi yake ikiongozwa na Mchungaji,
Mwenyekiti wa Mtaa na Mzee Maarufu ambaye ni Katibu wa Chama cha
Wakulima (TASO) kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Ramadhani Kiboko, huku
muafaka ukiwa haujapatikana.
Na EZEKIEL KAMANGA,wa KAMANGANA MATUKIO BLOG
Na EZEKIEL KAMANGA,wa KAMANGANA MATUKIO BLOG