m

"If you want to conquer fear, don't sit at home and think about it. Go out and get busy. "

-- Dale Carnegie, motivational expert

Tuesday, 9 October 2012

Israel na Mkristo

HOJA MPYA YA ASKOFU GAMANYWA--MAHUSIANO YA KIIMANI KATI YA MKRISTO NA TAIFA LA ISRAELI (SEHEMU YA 1)


Askofu Sylvester Gamanywa,Rais wa WAPO MISSION INTERNATIONAL.
      

Hivi karibuni nimetangaza mkakati maalum wa kuongoza misafara ya kuzulu Israeli. Misafara hii nimeipa jina la “ziara za kinabii katika Israeli”. Ziara ya kwanza itafanyika tarehe 9/7/2012 na itakuwa ya siku 12. Kwa kuwa ninafahamu kwamba, kuna utata wa kitheolojia uliochanganyikana na itikadi za kisiasa, nimeona niilete mada hii ili kutoa elimu sahihi, kuhusu “mahusiano ya kiima yaliyopo kati ya Mkristo na taifa la Israeli. Katika mada hii nakusudia kusimulia kwa ufupi historia ya maagano ya Mungu kwa Israeli na jinsi maaganoo hayo yanavyomgusa kiimani kila ajiitaye Mkristo, mpaka uchambuzi wa kiini cha utata wa kitheolojia kinachosababisha baadhi ya wakristo wasijue umuhimu wa kulinda  mahusiano ya kiimani kati ya na Israeli. Kwa leo nitaanza na historia fupi kuhusu maagano ya Mungu kwa Israeli na utendaji wake kiimani kwa mkristo halisi:

Agano La Mungu Kwa Ibrahimu

Japokuwa kihistoria katika Biblia kuhusu  maagano ilianza kwa Adamu na kisha kwa Nuhu. Tunapochunguza uzito wa maagano kati ya Mungu na binadamu, tunakuta unakuwa na uzito wa pekee kuanzia maisha ya mtu aliyeitwa Ibrahimu. Mungu anajieleza kwa Ibrahimu akimtabiria mambo makubwa yanayomhusu yeye binafsi na vizazi vyake vitakavyofuata baada yake. Tunapochunguza mchakato wa agano la Mungu kwa Ibrahimu tunakuta unaanza na wito, unafuatiwa na kiapo na utabiri wa mambo yajayo kwa uzao wa Ibrahimu:

1.       Wito wa Mungu kwa Ibrahimu
Historia ya Agano la Mungu kwa Ibrahimu inaanza ni wito maalum wa kutoka katika nchi yake, katika jamaa zake, na kuhamia katika nchi mpya ambayo angeoneshwa na Mungu mwenyewe.  Mungu anatoa ahadi maalum kwa Ibrahimu zitakazotokana na utii na uaminifu wake mbele za Mungu.

“Bwana akamwambia Abramu, toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpka nchi nitakayokuonyesha; name nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kuliza jina lako; nawe uwe Baraka; name nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.” (Mw.12:1-3)
Ukilisoma kwa  makini agano hili utagundua mambo muhimu matatu ambayo ni ahadi maalum zisizo na masharti ambazo Mungu alizitoa kwa Ibrahimu. La kwanza, ahadi ya nchi, pili ni ahadi ya uzao, na tatu ahadi ya Baraka.

2.       Kiapo cha Mungu cha agano na Ibrahimu
Baada ya Ibrahimu kutii wito na kuondoka nyumbani kwa baba yake na jamaa zake, wakati ameingia katika nchi ambayo Mungu alikuwa amekusudia kumpa, aliwasiliana naye ili kumhakikishia uaminifu wa ahadi zake. Ibrahimu aliomba ushahidi wa utumilifu wa ahadi za Mungu, na ndipo Mungu akaagiza dhabibu zitolewe ili wafanye agano:
“Kisha akamwambia, Mimi ni BWANA, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uirithi. Akasema ee Bwana MUNGU, nipateje kujua ya kwamba nitairithi? Akamwambia, unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua na mwana wa njia. Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua” (Mw.15:7-10)
Maandiko haya yashuhudia mchakato wa agano ulivyokuwa na ukihusisha kutoa dhabihu ya damu ya wanyama ambayo ni ishara kuwa ahadi zilizotolewa kulingana dhabihu lazima zitazimizwa.
Kimsingi, utaratibu wa agano hili ulikuwa ni lazima watu wawili wanaofanya agano wapiti katikati ya vipande viwili vilivyopasuliwa ikiwa ni ishara ya kila mmoja kujitoa mhanga wa kushika agano husika. Lakini katika mazingira haya, Mungu akitaka kuonyesha kuwa hili lilikuwa ni “agano lisilo na masharti” hakumruhusu Ibrahimu kupita katikati ya dhabihu. Badala yake tunasoma kwamba Mungu peke yake kwa ishara ya moto aliamua mwenyewe kupita katikati ya dhabihu hiyo: 
“Ikawa, jua lilipokuchwa ikawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka  ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Siku ile BWANA akafanya agano na Abramu, akasema, uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto Frati, Mkeni, na Mkenizi, na Mkadmoni, na Mhiti, na Mperizi, na Mrefai, na Mwamori, na Mkanaani, na Mgirgashi, na Myebusi.” (Mw.15:18-21)

3.       Ukomo wa Agano la Mungu kwa Ibrahimu
Aina ya agano la Mungu linaonesha kwamba ni la kudumu. Mungu alimhakikishia kwamba hilo litakuwa ni agano la milele, kutoka vizazi hadi vizazi vijavyo na halitabadilika wala kufikia ukomo. Mojawapo ya mambo ambayo ni ya kudumu ni “haki ya umilikaji” wa nchi ya Kanaani:
“Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako. Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa miliki la milele; name nitakuwa Mungu wao” (Mw.17:7-8)

4.       Mapito yajayo ya uzao wa Ibrahimu
Pamoja na kwamba, agano la Mungu kwa Ibrahimu halikuwa na masharti ya kumwajibisha, lakini liliweka bayana kuhusu mapito ambayo uzao wake utapitia.
Biblia ilitabiri kabla kwamba wa Ibrahimu ungelijikuta utumwani kwa kipindi cha miaka mia nne. Lakini baada ya hapo Mungu angekumbuka ahadi yakwe kwa Irahimu na kwenda kuwakomboa ili kuwaleta katika nchi aliyomwonyesha:

“BWANA akamwambia Abramu, ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali nyingi. Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa kwa uzee mwema. Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado.” (Mw.15:13-16)
Agano La Mungu Kwa Isaka
Wakati Mungu alipokuwa akiweka agano na Ibrahimu, bado alikuwa hana watoto wa kuwazaa mwenyewe. Siku moja Mungu alimhakikisha kwamba atampa mtoto wa kurithi agano la ahadi. Katika mahangaiko ya kibinadamu Sara alimshauri Ibrahimu amchukue Hajiri mjakazi ili ajipatie mtoto kupitia yeye.. Katika zoezi hilo akapatika mtoto wa kiume aliyeitwa Ishmael.
Wakati Mungu alipomtokea ili kuimarisha agano lake, Ibrahimu alimpendekeza Ishmael kuwa apokee mbaraka wa agano la ahadi kwa ajili ya vizazi vijavyo. Biblia imeandika msimamo wa Mungu kwa Ibrahimu kuhusu mtoto atakayekuwa mrithi wa agano la ahadi. Mungu hakumteua Ishmaeli akubeba wajibu huo maalum: Badala yake alipendekeza habari za urithi huo utatwaliwa na nani:
“Ibrahimu akamwambia Mungu,, lau kwamba Ishmaeli angeishi mbele yako. Mungu akasema sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Isaka. Nami nitafanya agano langu imara kwake kuwa agano la milele kwa ajili ya uzao wake baada yake. (MW.17:18-19)
Pamoja na kwamba Mungu hakumteua Ishmael kuwa mrithi wa agano la ahadi, lakini pia hakumtelekeza kabisa. Mungu alimpatia Ishmael mbaraka wake maalum ambao unadhihirisha kwamba yeye naye kabarikiwa na Mungu.
“Na kwa habari za Ishmaeli nimekusikia, nimembariki, nitamzidisha,  nami nitamwongeza san asana. Atazaa maseyidi kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kuu. Bali agano langu nitalifanya imara kwa Isaka, ambaye Sara atakuzalia majira kama haya mwaka ujao.” (Mw.17:20-21)

Kikapita kipindi cha mwaka ndipo Isaka akazaliwa. Hapo katikati yalipita mengi  lakini Biblia imeandika kwamba ulipofika wakati Ibrahimu kugawa urithi wake alitii agizo la Mungu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo:
“Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. Lakini wana wa Masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu.” (Mw.25:5-6)
Mwisho tunashuhudia Mungu akiwasiliana na Isaka moja kwa moja ili kulifanya imara agano lile alilolirithi kutoka kwa Baba yake:
“Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Ibrahimu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari. BWANA akamtokea, akasema, usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia. Kaa ugenini katika nchi hiyo, name nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako. Nitazidisha uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia. Kwa sababu Ibrahimu alisikiai sauti yangu, akayahifadi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu.” (Mw.26:1-5)
Agano La Mungu Kwa Yakobo
Historia ya Biblia imeandika jinsi ambavyo, Mungu alikuwa makini sana katika kuhakikisha anateua mtu anayestahili kurithi agano la ahadi alilofaanya na Ibrahimu. Tumekwisha kuona jinsi alivyomteua Isaka badala ya Ishmaeli. Sasa tunamkuta Mungu akiwa makini katika uteuzi wake.

Isaka alizaa watoto wawili wa kiume mapacha. Esau na Yakobo. Aliyetangulia kuzaliwa ni Esau lakini akifuatiwa na Yakobo akiwa ameshika kisigino cha Esau.
“Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake. Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau. Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake umashika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa.” (Mw.25:24-24)

Historia ya Biblia inaendelea kusimulia jinsi ambavyo mapacha hawa walikuwa na mambo kibinadamu yalitafsiriwa kuwa ujanja lakini yamadhihirisha kuwa ulikuwa ni ushindani wa kiimani, tena mabao Mungu aliufuatilia kwa karibu mpaka mwisho.
Jambo la kwanza, Yakobo kununua haki ya mzaliwa wa kwanza:

“Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani naye alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo tafadhali nipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu. Yakobo akamwambia, kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. Esau akasema, tazama, mimi ni karibu na kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? Yakobo akamwambia, uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake y amzaliwa wa kwanza.” (Mw.25:29-34)

Tukio la pili la aina yake ni pale ambapo Isaka alitaka kurithisha agano la ahadi kwa mtoto wake wa kwanza mbaye ni Esau. Inavyoonesha lile tendo la Esau kumuuzia Yakobo haki ya mzaliwa wa kwanza hazikuwahi kumfikia Isaka.
Lakini mkewe Rebeka tangu wakati akiwa mjamzito wa mapacha ya Esau na Yakobo alipata shida mpaka mimba hiyo mpaka akamwomba Mungu kuhusu hali hiyo. Na Mungu hakusita alimjibu kuhusu mambo yatakayowapata watoto atakaowazaa:
“Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA.  BWANA akamwambia, Mataifa mawili yako tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo. “(MWA. 25:22, 23)
Hapa tunahitaji kuzingatia mambo ya msingi yafuatayo. Kwanza, Rebeka alijua tangu kuzaliwa kwa Esau na Yakobo ni nani atachukua nafasi ya urithi wa Agano la ahadi. Haijulikani kama Rebeka alimwabia Yakobo siri hii au la. Pili, tukumbuke kwamba kisheria, Esau alikwisha kuipoteza haki ya mzaliwa wa kwanza kwa Yakobo. Lakini naye aliamua kupuuza. Yakobo aliamini kwamba kisheria yeye ndiye mzaliwa wa kwanza badala ya Esau, japokuwa baba yake Isaka hajui yote hayo.
Watafsiri wengine wa maandiko wanadhani kwamba Yakobo na mama yake wote waliijua siri hii ya nani anastahili kupokea mbaraka wa mzaliwa wa kwanza. Ndiyo maana hoja haikuwa kwa nini wanafanya hila, bali hofu ya kugundulika kwa hila yenyewe kabla na Isaka.
Biblia haikuficha ukweli wa suala zima badala yake imeandika jinsi mbinu ilivyofanyika baada ya Esau kwenda kuwinda mnyama wa kumwandalia Isaka chakula; huku nyuma mama yake Yakobo akamwandalia mwanawe chakula ili awahi kumpelekea Isaka kabla Esau hajarudi.
Zoezi hilo lilifanikiwa. Yakobo akawasilisha chakula kwa Isaka baba yake, na baada ya mahojiano mengi, hatimaye Isaka akaachilia mbaraka wa mzaliwa wa kwanza kwa Yakobo badala ya Esau:
“Akakaribia akambusu. Naye akasikia harufu ya mavazi yake, akambariki akasema, Tazama, harufu ya mwanangu. Ni kama harufu ya shamba alilolibariki Bwana. Mungu na akupe ya umande wa mbingu, Na ya manono ya nchi, Na wingi wa nafaka na mvinyo. Mataifa na wakutumikie, Na makabila wakusujudie, Uwe bwana wa ndugu zako, Na wana wa mama yako na wakusujudie. Atakayekulaani alaaniwe, Na atakayekubariki abarikiwe. (MWA. 27:27-29)
Maswali magumu yameulizwa kuhusiana na tukio hili. Je! Mungu aliridhia mbaraka huu ambao mtoaji hakuwa anajua anambariki nani? Kama ndiyo, je! Mungu naye ameshiriki kubariki hila ili mbaraka uende kwa asiyehusika?  Kumbuka maswali haya yanamhusu Mungu moja kwa moja, na vile ambavyo alilichukulia tukio hili.
Lakini kama tulivyokwisha kusoma huko nyuma, Biblia inaweka wazi msimamo wa Mungu tangu mwanzo kuhusu suala hili. Pamoja na kwamba, mchakatp mzima wa Yakobo kuupata mbaraka umejaa utata mtupu mbele za Mungu; kinachozingatiwa ni kile kilichokwisha kutabiriwa na Mungu mwenyewe kabla ya kuzaliwa kwa wahusika. Isitoshe, Mungu aliridhia Yakobo kupokea mbaraka huo sio kwa ujanja uliotumika, bali kwa sababu alikwisha kustahili kwa mujibu wa sheria. 
“Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu, (kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo bali kwa sababu ya nia yake aitaye,) aliambiwa hivi mkubwa atamtumikia mdogo.” (Rum.9:10-12)
Biblia pia imeandika yote yaliyojiri baada ya Esau kurudi na kukuta tayari Yakobo ameshateka mbaraka!  Biblia pia inasimulia jinsi Isaka alivyoshtuka baada ya kugundua aliyechukua mbaraka ni Yakobo na si Esau aliyemkusudia tangu mwanzo. Hata hivyo, Isaka alikuja kumsamehe Yakobo na kuamua kwa hiari kumbariki rasmi:
“Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani.  Na Mungu Mwenyezi, akubariki, akuzidishe, na kukuongeza, ili uwe mkutano wa makabila.  Akupe mbaraka wa Ibrahimu, wewe na uzao wako pamoja nawe, upate kuirithi nchi ya kusafiri kwako, Mungu aliyompa Ibrahimu.” (MWA. 28:1-4)

Hii kwa chanzo cha Gospel Kitaa.blogspot.com

No comments:

Post a Comment