TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) KUHUSU KUVULIWA NAFASI ZAUONGOZI NDANI YA CHAMA CHANGU CHA CHADEMA
1. Utangulizi
i. Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe
20 - 22 Novemba 2013, Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine,
iliazimia kunivua nafasi zangu
zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa taarifa ya chama iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari
siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba
2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk Kitila
Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka unaojulikana kama
mkakati wa uchaguzi 2013. Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama
ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu . Sababu za kufukuzwa
kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa
ndani na nje ya vikao vya chama. Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na
CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha
tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao
mbalimbali vyama.
ii.
Ninatambua kwamba chama changu kinapita
katika wakati mgumu sana sasa hivi.
Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo
cha CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu
atakapokuwa mtu mzima na atakapoamua
kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na chama changu na ninaamini ndicho
kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.
2.
Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu
Zipo
tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu.
Tuhuma hizi zinalenga kuonyesha kwamba
mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili kukihujumu chama changu. Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu
kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea
wetu wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo
kuhusu jambo hili:
● Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko
Kigoma.
●
Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16 katika mikoa
mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara
na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika
majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
● Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani,
ubunge na Rais.
●
Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa
kuwapigia kampeni wagombea wetu
kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika uchaguzi huo. Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea
wetu, na hivyo ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua.iii) Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea
wetu katika baadhi ya majimbo
kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo
yanayotajwa ni pamoja na Sumbawanga,
Musoma Vijijini na Singida Mjini. Kama nilivyokwisha kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli
na hakuna popote ambapo watoa tuhuma
hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba nilifanya jambo hili. Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na
ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya
kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi
wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.iv) Tuhuma kwamba nimekuwa
sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama: Ukweli ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni
mbalimbali za chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa katika mikoa ya
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa yote
tuliyotembelea. Mwaka 2012 baada ya
hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na operesheni kubwa moja katika mikoa ya
kusini ya Mtwara na Lindi. Operesheni
hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa mwaliko
wa Watanzania wanaoishi huko.v)
Tuhuma
kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG):
Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu nilipaswa
kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya'
ili wajiandae. Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na
kukiweka kundi moja na CCM na nastahili
kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo
ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:
●
Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni
kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania
kuzibadilisha
●
Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa
nje kwa utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni
kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa
la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.
vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu
kuchukua Posho za Vikao
Mtakumbuka
kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa
kupinga posho za kukaa na matumizi
mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba hivi
karibuni Mheshimiwa Lema amenishutumu
kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya
umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza
yafuatayo kuhusu jambo hili:
●
Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu mwaka 2011. Hii ni
pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge ninavyohudhuria. Mtu
yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani
.● Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la
kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala la kimisingi zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina
mama wajawazito ni 1900 kati ya
wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa
huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi
ya Serikali katika Ilani, na kuondoa
posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa, kungesaidia
sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.
●
Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.3 Usambazaji wa Ripoti ya
Siri kuhusu Zitto Kabwe. Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya
siri kuhusu mimi ukibeba lundo la tuhuma
kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu ya
CHADEMA. Jambo hili pia lilijadiliwa
katika kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu haukuandaliwa wala kusambazwa na
makao makuu. Katika mchango wangu nililalamikia mambo matatu
yafuatayo:i. Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza
waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini
kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa
taratibu za chama chetu.ii. Kwa kuwa chama
kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote
waliohusika kutengeneza hekaya ile wanachukuliwa hatua stahiki za
kisheria.
4.
Hitimisho
a) Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu
mapigo na ningewazodoa
watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za Tanzania. Natambua
pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya siasa
hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'. Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata
nafasi ya kuendelea kutumia suala
hili katika harakati zao za kudhoofisha mapambano ya demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani
nchini mwetu
Napenda wanachama wa CHADEMA
na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini
watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu
wa chama hiki na nitakuwa wa
mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote
ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.b)
Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na
zinanikwaza. Tuache siasa za uzushi
ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania wenye
matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.
c) Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda
sasa yapo mengi mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa
na yapo makosa niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.
d) Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya
kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina,
waumini wa uwajibikaji dhidi ya
wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka. Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama
chetu inayohitaji uongozi shupavu
kuikabili. Nitasimama daima upande wa demokrasia. Kama alivyopata kunena
mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha uzalendo katika nchi
ni kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni
wa chama chetu.
Kabwe
Zuberi Zitto, Mb
Dar
es Salaam.24 Novemba, 2013
Video