Pendekezo la Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kwa serikali ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo izungumze na makundi ya waasi na nchi jirani
kutatua mzozo wa mashariki ya nchi hiyo linaonekana kuwagawa Wakongo.
Kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa, kuna
mwangwi wa sauti za Wakongomani wakiupongeza msimamo wa Rais Kikwete
kwamba kuweko na mtazamo wa ujumla katika kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa
kanda ya Maziwa Makuu.
Mwandishi wetu wa Kinshasa anaripoti kwamba wakaazi wengi wa mji huo
wanaamini kuwa pendekezo hilo la Rais Kikwete linaweza kusaidia amani ya
kudumu.
Kwenye mkutano wa marais 11 wa Nchi za Maziwa Makuu kwa ajili ya Kongo
uliotishwa kando ya mkutano wa Umoja wa Afrika, mjini AddisAbaba, Rais
Kikwete alipendekeza kufanyike mazungumzo baina ya Kongo na kundi la
waasi la M23, Rwanda na kundi la waasi la FDLR na Uganda na waasi wake
wa ADF/Nalu kwa ajili ya amani ya kudumu ya kanda ya Maziwa Makuu.
Tanzania inachangia wanajeshi 1,280 kwenye kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa mashariki mwa Kongo,
Umoja usio wa kawaida Kinshasa
Rais Paul Kagame wa Rwanda (kushoto) na Joseph Kabila wa DRC.
Pendekezo hili limezua kile mwandishi wetu wa Kinshasa
anachokiita “tukio la nadra kabisa nchini Kongo“ kwa wabunge wa upinzani
na wale wa chama tawala kuwa na kauli moja kuhusu maswala muhimu ya
kitaifa.
Rais Kikwete amefanikiwa kuwaelekeza wanasiasa wa Kongo kuchukuwa
msimamo wa pamoja kuhusu juhudi za kutafuta suluhisho la kudumu kwenye
kanda ya Maziwa Makuu.
Kwa mujibu wa taarifa za mashirika ya habari ni kwamba Rais Kikwete
aliwambia maraisi wenzake pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban
Ki-moon, na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Afrika, kwamba
ni lazima kuweko na mtizamo wa ujumla kwa ajili ya kumalizisha machafuko
ya miaka mingi kwenye kanda la Maziwa Makuu.
Kwa hiyo Rais Kikwete alipendekeza Kongo kuendesha mazungumzo na waasi
wa M23, na vilevile kuitaka Rwanda kuzungumza na waasi wa FDLR na Uganda
kufungua mazungumzo na waasi wake wa ADF/Nalu. Pendekezo hilo
limepongezwa na upinzani na chama tawala nchini Kongo, akiwemo mbunge
Justin Bitakwira, ambaye ni kiongozi wa wabunge wa upinzani wa UNC.
Naye Franklin Tshamala, msemaji wa muungano wa vyama tawala, amesema
kwamba pendekezo hilo la Rais Kikwete ni hatua ya ujasiri ya kutaka
kurekebisha mitizamo tofauti waliyonayo viongozi wa mataifa haya matatu.
Rwanda yakataa
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC.
Pendekezo hilo la Rais wa Tanzania lilipongezwa pia na
serikali ya Kongo. Akiwa mjini Addis Ababa, Waziri wa Mambo ya Nje ya
Kongo, Raymond Tshibanda, aliiambia Radio France Internationale kwamba
msimamo huo unalingana na ombi la miaka mingi la serikali ya Kongo kwa
majirani zake.
Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo, aliyehojiwa
na redio hiyo hiyo alisema matamshi hayo ya Rais Kikwete ni ya upotofu
na nchi yake haiwezi kamwe kuzungumza na watu waliohusika na mauwaji ya
halaiki.
Magazeti mengi ya siku ya Jumanne (tarehe 28 Mei) yamezungumzia matamshi
ya Rais Kikwete na maoni ya wananchi wa Kongo. Gazeti Lavenir
limechapisha kichwa cha habari kwa wino mzito kikimuita Rais Kikwete
”Jjasiri wa kanda ya Maziwa Makuu.”
Kwenye ukarasa wa mwanzo, gazeti la upinzani la Tempetes des Tropiques
limeandika “Kikwete arusha bomu Addis Abeba”, likiyaelezea matamshi ya
Rais Kikwete kuwa sawa na bomu alilowarushia marais wenzake ambao kwa
muda mrefu wameonyesha unafiki katika kumaliza machafuko ya Maziwa Makuu
kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Goma hawataki mazungumzo na M23
Wakimbizi wa ndani mashariki ya Kongo.
Lakini hali ikiwa hivyo mjini Kinshasa, kwenye eneo la
mashariki ya Kongo, ambako ndiko hasa kwenye mgogoro kati ya serikali na
waasi wa M23, maoni ni tafauti.
Mwandishi wetu wa Goma, John Kanyunyu, anaripoti kwamba mashirika ya
kiraia ya huko yamekataa mazungumzo baina ya serikali ya DRC na wajumbe
wa M23.
Makamu mwenyekiti wa mashirika ya hayo kiraia katika mkoa wa Kivu ya
Kaskazini, ambaye pia ni msemaji wa mashirika hayo, Omar Kavota, amesema
“hakuna tena la kuzungumza, kwani tayari mkataba wa M23 baina ya chama
cha zamani cha uasi CNDP umeshajadiliwa.”
Kauli hiyo ya mashirika ya kiraia inakuja baada ya pendekezo la Rais
Kikwete mbele ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na marais wa kanda ya
Maziwa Makuu kuiomba serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo baina
yake na waasi wa M23.
Aidha kauli hiyo ya mashirika ya kiraia ya kuitaka serikali kutozungumza
na wajumbe wa M23, inachochewa pia na utendaji kazi wa wanajeshi wa
serikali katika uwanja wa mapigano.
Katika vita baina ya jeshi la serikali, FARDC, na waasi wa M23, jeshi
hilo la serikali linatajwa kuwa, lilifaulu kwa mara ya kwanza kabisa,
kuwazuia waasi wa M23 kuuteka upya mji wa Goma.
Kavota anasema ni bora zaidi kuwapatia nafasi ya kufanya kazi zao
wanajeshi wa kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa kinachowajumuisha
wanajeshi kutoka Tanzania, Malawi na Afrika ya Kusini.
Katika kuwapongeza wanajeshi wa serikali kwa kazi waliyoifanya wakati wa
mapigano ya wiki iliyopita, mashirika ya wanawake kutoka asasi za
kiraia na vyama vya kisiasa, wametoa mchango wa pesa wa kile
walichokiita “kuwanunulia wanajeshi wa serikali maji ya kunywa.”
Ripoti hii imetayarishwa na Saleh Mwanamilongo, Kinshasa, na John Kanyunyu, Goma
Mhariri: Mohammed Khelef