Unahitajika Utafiti wa Kina Juu ya Ufaulu wa Wanafunzi
Ndugu watanzania hivi karibuni kumeibuka sakata kubwa kabisa juu kufeli mtihani wa taifa wa kidato cha nne wa mwaka 2011 kwa wanafunzi wengi . Binafsi nimekuwa kimya nikibaki kushuhudia mabishano makubwa katika jamii. Kila mmoja amekuwa na mtizamo wa kwake, ingawa kunaibuka makundi kama matatu hivi; la kwanza ni lile linalolaumu ukosefu wa walimu na moja kwa moja huzitaja shule za kata, la pili ni lile linalolaumu usahishaji likilenga moja kwa moja baraza la Mitihani la Taifa(NECTA) na la tatu na ambalo linaonekana dhaifu ni linaloona kushuuka kwa maadili ya mwanafunzi( kwa mtazamo wangu hili lilipaswa liheshimiwe zaidi). Kitaaluma mimi ni mwanafunzi wa chuo kikuu ninayechukua shahada ya kwanza ya Sanaa na Elimu(BAEd) na ikumbukwe kabla ya hapo nimekuwa mwanafunzi wa sekondari na msingi. Nina sehemu fulani ya uzoefu juu wa wanafunzi,walimu, shule na hata matokeo ya mitihani. Ninavyoelewa watanzania wengi ukiwaruhusu waongee watakushinda tu lakini utakapohoji walete hoja na visibitisho wataweka mikono mfukoni na kuona soga limewashinda.
Natamani kuweka sawa katika sababu zilizopelekea kushuka kwa ufaulu wanafunzi kuwa hauhitaji porojo kwani ni suala muhimu linaloibeba Tanzania ya kesho, kama tutalifanyia porojo, mzaha na hata siasa basi tujue tutakuwa tumekumbatia bomu lililochakaa ambalo litalipuka wakati wowote. Binafsi nashauri UTAFITI wa kina kabisa ufanywe na matokeo ya utafiti yafanyiwe kazi. Naenda mbali zaidi kwa kusema utafiti ulenge kwanza kuangalia uwezo wa wanafunzi wenyewe (personal ability) kwa sababu nawaona wanafunzi wa kileo wamesheni mambo mengi kama vile simu zilizojaa picha chafu, facebook na muziki wa kimagharibi kwa wingi lakini pia wanaratiba za ligi zote za Ulaya na wanajitahidi kutazama mechi zote. Wanafunzi hao hao utakuta wakilaumu mwalimu aliyejitoa kuwa fundisha siku ya ziada ya jumamosi kwa sh. 200 au bure kabisa wakati wanapoteza dakika.105-130 pamoja na sh.500 kutazama mechi moja au kwenda intenet cafe sh. 1000-1500 kwa saa. Bado mwanafunzi huyo wakati wote utamuona ama akitikisa kichwa au kunesanesa wakati wote akiimba nyimbo fulani na pia mwanafunzi huyohuyo kajawa na lugha za matusi, dharau na chuki juu ya walimu. Je mwanafunzi huyo ataweza vipi kufaulu wakati mapema kajibebesha mizigo ya kutosha? Lakini pia vitu hivyo kafundishwa nani hata asingizie walimu kutofundisha ndo sababu ya kufeli? Hizi ndizo sababu zinazopelekea mwisho wa siku mwanafuzi ashindwe cha kujaza kwenye mtihani na hivyo kuandika VILIVYOMJAA MOYONI- MATUSI, MICHORO YA KIHUNI NA MIZIKI. Si Dkt Joyce Ndalichako alituonyesha baadhi ya vituko? Uwezo binafsi wa mwanafunzi una mchango mkubwa kwa ufaulu mfano hai ni Yule mwanafunzi wa huko Songea ambaye alipata daraja la I wakati shule nzima haikuwa na daraja linguine la I,II na III aliwezaje kuibuka shujaa pia shule nyiongi kongwe za bweni zina walimu wachache lakini wanafunzi wake hujitoa mhanga kusoma kwa bidii hata kubaki shule wakati wa likizo ili tu waweze kukamilisha mitaala kwa jitihada binafsi.
Mlengwa wa Pili ni Mzazi wa mwanafunzi, je anafuatilia anachojifunza mwanae. Wazazi wa siku hizi wako bize na kazi zao, soga,bao, soka la ulaya, saloon. Wanakumbuka tu kulaumu matokeo yanapotoka aidha wawatukane wanawe, walimu au baraza lakini maji yanakuwa yamemwagika. Wazazi wasasa wanataka watoto wao walelewe kisasa bila kuadhibiwa au kuamrishwa kwa namna yoyote na hili limepelekea kutofautiana kwa malezi ya mwalimu na mzazi juu ya mwanafuzi. Hapo awali mzazi hata kama hajui kusoma aliwajibika kutazama maendeleo ya mwanae kila siku japo kuangalia pata(V) na kosa(X) na alipoona kosa nyingi alimuwajibisha kwa viboko maridhawa. Lakini sasa ukichapa kiboko mwanafunzi mzazi anakuja juu kwa mfano mwaka jana pale Ilala kuna shule mwalimu alipelekwa mahabusu na mzazi kwa kosa la kumchapa mwanae viboko vitatu. Mzazi ana mchango muhimu kwa maendeleo ya mtoto kwani ndiye anayesikilizwa na mwanafunzi kuliko mtu yeyote.
Mlengwa wa tatu awe mwalimu, nasisitiza kuwa awe mwalimu na si idadi ya walimu. Huyu mwalimu wa sasa tumchunguze uwezo wake binafsi, elimu yake, wito na mahitaji yake. Nina shaka na uwezo wa baadhi ya walimu, pita katika taasisi mbalimbali za elimu na uchunguze walimu wanaojiendeleza utashangaa kukuta wakihaha japo tu kutafsiri masomo yao ya msingi( definitions of their basic subjects) ukimuuliza inakuwaje mambo ya kawaida katika somo lake asiyajue? Jibu litakuwa kwani hujui chuo ni kuanza kila kitu. Lakini mwalimu huyo huyo asiyejua tafsiri tu somo lake utakuta ndiye mwalimu mkuu wa somo(subject master) katika shule anayofundisha. Lakini bado mwalimu huyo utakuta kapata elimu isiyo bora kwa mfano kuna walimu wa sayansi ambao wamesoma shule na vyuo visivyo na maabara, kama mwalimu huyo alisoma katika elimu ya hovyo pia atatoa elimu ya hovyo zaidi. Tatu ni ule wito; walimu wengi sasa wanasomea ualimu kama taaluma tu na si wito tena mfano halisi ni mfumo wa sasa wa kumpata mwalimu; mwanafunzi aliyekosa kwenda kidato cha tano,chuo kikuu au mkopo ndo hulazimika kukimbilia chuo cha ualimu au shahada ya elimu hivyo kufanya ualimu kuwa jalala la waliokosa taaluma walizohitaji ama wasio na vigezo vya kupata mkopo. Hapo hatuzalishi walimu bali wapita njia katika ualimu na sidhani hata kidogo kama wataweza kutoa elimu safi kwa mwanafunzi. Ni ukweli usiopoingika kuwa zaidi ya nusu wanafunzi wa elimu wamefuata mikopo tu ni si wito wao. Ni mwisho kwa mwalimu ni mahitaji stahiki, mwalimu wa zamani alithaminiwa na jamii kwa sababu serikali yenyewe ilimthamini. Mwalimu naye anamahitaji yake muhimu kama nyumba nzuri, chakula, usafiri na hata mazingira mazuri ya kazi lakini utaona ni tofauti kabisa hii inamfanya mwalimu kutothamini kazi yake na kupelekea kutoa elimu ya hovyo au kutofundisha kabisa au kufundisha tuisheni ili akidhi mahitaji yake. Ikumbukwe mwalimu ana mahitaji sawa kabisa na madaktari japo hagomi kama wao kuna wasiwasi kuwa wanagoma mioyoni mwao jambo ambalo ni hatari kwani ni vigumu kubaini mgomo wa moyoni.
Mlengwa mwingine wa kutazamwa iwe mazingira ya elimu na shule zenyewe, mazingira mabovu ya kusomea yaliyojaa ubaguzi pia yanachochea wanafunzi kufanya vibaya hebu tufikiri mbona matokeo ya baadhi ya shule kama Kibaha, Iliboru na hata Mbeya sek suala la matokeo mabovu haliwakumbi sana wakati nazo ni shule za serikali? Ni ukweli kuwa zina mazingira bora ya mwanafunzi kufanya vizuri na idadi ya walimu yenye uwiano. Ajabu ni kuwa kuna baadhi ya shule kongwe ambazo kabla uhuru na wakati wa utawala wa awamu ya kwanza zilikuwa na mazingia bora kabisa lakini kila uchao maabara na maktaba zao zinazidi kubadilishwa matumizi. Mfano, halisi ni ile shule kongwe ya Kantalamba sekondari- Sumbawangasasa haifanani hata na baadhi ya shule za kata kwani kila kitu pale kina hali mbaya kabisa. Wanafunzi watawezaje kufaulu katika mazingira hayo?
Mlengwa mwingine awe jamii yote kwa ujumla, jamii ya sasa inavumilia kuona maovu yanayofanywa na wanafunzi hata wakati mwingine kuyashangilia. Taaluma inaenda sambamba na nidhamu na suala hili la nidhamu ni la jamii nzima. Jamii isiwe tayari tu kulaumu matokeo bali ijihusishe kikamilifu katika malezi ya wanafunzi mara tu wanapoachana na walimu wao. Zamani suala la malezi lilikuwa la jamii nzima lakini sasa utandawazi unatumika vibaya kuharibu mfumo huo wa malezi.
Na mwisho ndio tunaweza kuchunguza serikali na vyombo vyake muhimu vya elimu, wizara, Taasisi ya Elimu Tanzania, Baraza la Mitihani la Taifa, malaka ya Elimu n.k maana utendaji wao pia unaweza ukawa na shaka kama vile kuvuja kwa mitihani na usimamizi mbovu. Japo jambo linalofanywa na katibu wa Baraza la Taifa la Mitihani Dkt. Joyce Ndalichako la kuonyesha madudu yanayofanywa na wanafunzi ni uwazi safi wenye kupunguza mabishano katika jamii juu ya nini wanafunzi wanafanya.
Huu ndio mtizamo wangu juu ya ufaulu wa wanafunzi na sababu zinazoweza kupelekea kufeli kwao na mtu yeyote anaweza kuupitia hata kuupinga kwani si utafiti hasa ambao umepitia njia za kisayansi za utafiti( scientific methods). Wito wangu ni kwa vyombo vyote vikereketwa vya elimu na utaifa kufanya utafiti wa kina wa kisayansi na kutupa majibu, na serikali ifanyie kazi majibu ya utafiti mbalimbali ikiwa utafanyika ili kuliokoa Taifa.
Wenu
Peter Kapagi
SJUT-Dar es Salaam
Simu ya kiganjani; +255 764 734620