Kwa ufupi
- Serikali kwa nyakati tofauti imejaribu kuweka msisitizo wa ufundishaji kwa kutumia lugha ya Kiingereza bila mafanikio. Mfano mzuri ni mradi ujulikanao kwa jina la English Language Teaching Support Project 1996-2000 (ELTSP).
Leo nahitimisha mfululizo wa makala zangu kuhusu
sababu za anguko la elimu nchini na namna tunavyoweza kunusuru
mustakbali wa elimu yetu. Endelea…
Serikali kwa nyakati tofauti imejaribu kuweka
msisitizo wa ufundishaji kwa kutumia lugha ya Kiingereza bila mafanikio.
Mfano mzuri ni mradi ujulikanao kwa jina la English Language Teaching
Support Project 1996-2000 (ELTSP).
Mradi huu ni miongoni mwa mikakati iliyoshindwa
kutuletea manufaa katika ufundishaji wa lugha ya Kiingereza shuleni kama
lugha ya kufundishia. Ifike wakati tukubali sasa kuwa tunahitaji
kufanya uamuzi mgumu na wenye gharama kwa manufaa ya taifa letu.
Idara ya Ukaguzi ndicho chombo chenye mamlaka ya
kusimamia ubora wa elimu itolewayo nchini. Hata hivyo, idara hii imekuwa
ikikabiliwa na changamoto nyingi, jambo linalosababisha ishindwe
kutimiza wajibu wake ipasavyo.
Kuna haja ya kudurusu upya majukumu ya idara hii
ili pamoja na mambo mengine, miongozo na mipango katika ukaguzi wa shule
itoe kipaumbele katika matokeo ya wanafunzi.
Ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2008, inaeleza wazi kuwa
ukaguzi shuleni umeshindwa kusimamia utoaji wa elimu bora.
Kuna haja ya Serikali kuangalia uwezekano wa
kuifanya idara ya ukaguzi wa shule kuwa taasisi inayojitegemea kama
zilivyo taasisi nyingine za elimu. Aidha, muundo na utendaji wake
viangaliwe upya ili kuipa nguvu idara hii.
Ninaamini idara hii ikiwezeshwa kwa kupewa hadhi
ya kuwa taasisi au hata mamlaka kamili, upo uwezekano mkubwa kuwa sasa
shule zetu zitakuwa na nafasi kubwa ya kukaguliwa mara kwa mara. Kwa
hakika tunahitaji kuwa na shule zinazokaguliwa.
Wajibu wa wadau wa elimu
Katika muktadha wa mjadala huu, wadau wa elimu ni
pamoja na waajiri, wazazi, walimu na wanafunzi. Kila mmoja kati ya hawa
ana wajibu wa kujenga mustakabali wa maendeleo ya Taifa, kwa kuhakikisha
anatimiza wajibu wake kikamilifu.
Mwajiri kwa mfano, anapaswa kuhakikisha kuwa
mwalimu anajengewa uwezo na mazingira bora yatakayo mwezesha kutekeleza
wajibu wake akiwa na moyo mkunjufu.
Aidha, wazazi na jamii kwa jumla ni kiungo muhimu
sana katika kuinua kiwango cha elimu hapa nchini. Hii inatokana na
ukweli kuwa mwanafunzi ni zao la jamii husika na ndiko anakotumia muda
mwingi katika ukuaji wake nje ya shule.
No comments:
Post a Comment