Monday, 17 December 2012

Kupata na kutembea katika kibali



16.12.2012, Ziara ya CASFETA-SJUTDSM kanisa la EAG(T)-Buguruni Kisiwani, Dsm
Kibali ni hali ya kukubalika, kuthibitika(approval) na kuwa na Baraka na fadhila za pekee katika maisha. Na kutafuta kibali ni hali ya kuhitaji kupata kukubalika, kuthibitika na kupata Baraka na fadhila za pekee katika maisha. Kibali kina uhusiano wa karibu na huruma na neema.
Kupata kibali kwa Mungu na Bwana wetu Yesu Kristo kunategemea ridhaa(Pleasure) ya Mungu mwenyewe na kinaweza kuongezwa(extended) kwa kuishi kwa haki na maombi. Kwa hiyo tunaona kuwa kibali kinaweza kuja moja kwa moja yaani mtu anazaliwa nacho lakini pia maisha ya haki au utakatifu na maombi yanaweza kumwezesha mwamini kupata kibali. Kwa mfano Musa (Kutoka 33:12-13) alizaliwa na kibali hata pale alipotupwa majini bado alionekana na si kwa watu masikini lakini watu wakubwa kabisa katika nchi, kibali chake hakikuweza kuzuiwa na mtu yeyote katika maisha yake, na hata mauti ilipata kibali kiasi cha kuzikwa na Mungu Mwenyewe…kutembea na kibali ni raha sana, na kama utaweza kujifunza kwa watu kadhaa katika biblia waliopata na kutembea na kibali hutachoka kuisoma Biblia, hutaichoka imani yako na hautachoka kuomba maana moyo wote utavutwa kuhitaji kibali cha Mungu.
Kupata kibali ni jambo moja na kutembea katika kibali ni jambo lingine, unaweza kuzaliwa na kibali cha Mungu lakini usitembee katika kibali hicho isipokuwa kwa uhitaji wa kibali, maombi na bidii ya kutafuta kibali. Kwa kweli kutafuta kibali ni jambo la msingi kwa mwamini kwani linaleta raha ya wokovu na wepesi wa msalaba na hivyo kuchochea imani na bidii ya utakatifu. Kibali kinalipa katika maisha, kwa mfano Yusufu na Danieli walipata uwaziri mkuu si kwa vigezo wala uwezo bali kwa kibali pekee, Daudi alipata Ufalme sababu alitembea katika kibali, Nehemia aliweza kujenga ukuta wa Yerusalemu uliobomoka kwa sababu ya Kibali, Esta naye akawa Malikia katika nchi ya utumwa kwa sababu ya kibali. Kibali ni kwa ajili ya huduma yako, kibali ni kwa ajili ya kazi, masomo, uongozi, na maisha yako yako ya kila siku, kibali ni ushindi wako, na jamaa zako. Ukipata kibali hakika hata ndugu zako watafaidi, majirani wataoga katika baraka zako na kila eneo utakalokuwepo litanufaika kwa wewe kutembea katika kibali. Kwa hiyo kutotembea katika kibali si kwamba unajinyima mwenyewe bali unawanyima haki hata ndugu, majirani na wafanyakazi wenzako kwani Bwana anataka kutupa kibali kwa ajili yetu na wengine, tukisoma Mwanzo 12:2 inasema …nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako, nawe uwe Baraka( maana yake ufanyike Baraka kwa wengine).
Tunza kibali na tembea katika kibali. Kupoteza kibali ni kupoteza kila kitu.
Hebu tupitie watumishi wa Mungu waliofaidi na kufurahia kutembea katika kibali cha Mungu;
1.      Yusufu, kwa kweli namuona ndiye mtu aliyepata kibali cha pekee (Supernatural favor) kwa kuyatazama maisha ya Yusufu kuzaliwa, kuuzwa, kuishi gerezani, kuwa waziri mkuu na kuwafadhili wana wa Israeli wakati wa njaa (Mwanzo sura ya 37-50), tukisoma mwanzo 39:1-5 …5Mbaraka wa Bwana ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba…
2.      Abram/Ibrahimu, huyu ndio aliahidiwa kubarikiwa hadi uzao wake. Neno lenyewe latosha kueleza kibali chake kwa wakati Mwanzo 12:2 Bwana anamuahidi Kibali Ibrahim Mwanzo 13:2 inathibitisha kibali na kwamba alitembea katika kibali naye Abraham alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha na kwa dhahabu pia sura ya 24:1 inasema b Bwana  alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote.
3.      Daudi, hata simba na dubu walitambua kibali chake lakini kibali chake hakikuonekana hadi alipofanya kazi ya kumwua Goliathi. 1Samweli 18:6-7
...Sauli ameua elfu zake,
  Na Daudi kumi elfu zake.  
Wanawake waliimba hivyo na kuthibitisha kibali cha Daudi kuliko Sauli. Daudi alitembea na kibali tangu akiwa kijana hadi ufalme, hata ufalme wake ulipata ushindi kwa kila vita.
4.      Danieli; Nabii aliyeishi utumwani Babeli lakini kwa kibali cha Mungu hata kupata uwaziri mkuu wakati hakuwa na kigezo chochote cha kushika wadhifa wa juu Babeli. Danieli 1:9 Basi Mungu akamjalia Danieli kupata kibali na huruma machoni pa huyo mkuu wa matowashi. 6:3 basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake(ni roho ya kibali), naye mfalime akaazimu kumweka juu ya ufalme wote.
5.      Esta, Naye kama Daniel alikuwa katika nchi ya ugeni akilelewa na Mordekai mara wazazi wake walipofariki, pamoja na kuwa mateka lakini alifanikiwa kuingia katika mashindano ya kutamfuta malkia wa mfalme Ahasuero na akashinda   (Esta 2:5-17) mstari wa 15b unasema naye huyu Esta alikuwa amepata kibali machoni pa wote waliomwona. Na 17 inaongeza mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote. Utaona kuwa Esta alikuwa na kibali ambacho kikamwezesha kukubalika na hata kuthibitika mbele ya watu wote na mfalme. Tangu zamani hata leo mfumo wa utawala hauruhusu mtu asiye mzawa kushika nafasi ya juu ya uongozi lakini Esta alifanikiwa tena akapendwa kuliko wanawake wote. Kibali kinafanya mtu apendwe mahali popote na watu wote, kibali kinamfanya mtu awe na mvuto wa sura, maongezi na kazi yoyote afanyayo. Kibali ni raha sana kwa mwamini, naweza kusema ukitembea na kibali utaishi popote na kwa nafasi ya pekee.
Muda huu wa ibada moja hautaweza kutosha kama tutataja watu wote waliotembea katika kibali cha Mungu… lakini ni vyema kujua ni muhimu kutafuta kibali kwa Mungu na kutembea katika kibali hicho.
Unaweza kupata kibali kwa maombi kama Musa alivyoomba neema (Mwanzo 33:12­-13) na Neno linasema katika Zaburi 84:11 Kwa kuwa Bwana Mungu ni jua na ngao, Bwana atatoa neema na utukufu. Hatawanyima kitu chema hao waendao kwa ukamilifu. Kuna jambo lingine linaloweza kumpatia mtu kibali ambalo ni Ukamilifu, kuishi maisha makamilifu ya haki na utakatifu.
Pia kibali yaani kukubalika na hata kuthibitika kunaweza kupatikana kwa uaminifu na huduma njema, Yusufu alipata kibali kwa Potifa kwa sababu alitawala vizuri nyumba yake… ni kweli alizaliwa na kibali lakini kilithibitika kwa kuwa mwaminifu na bidii ya kazi kwa Potifa. Ruthu alitafuta kibali kwa mumewe Boazi kwa kumfanyia ukarimu mkwewe Naomi(Ruthu 2:2). Na Na hata Daudi kibali chake kilianza kuonekana mpaka pale alipojitosa kumpiga Goliathi.
Mwamini yeyote asimame kwa miguu yake mwenyewe aombe kibali kwa mungu kwa ajili ya kila jambo… ukipata kibali hakuna jambo litakalokwama. Kibali ni kwa ajili yako, kazi yako, majirani zako, ndugu zako na zaidi kwa jili ya utukufu wa Mungu.
Isaya 60:1
Ondoka uangaze kwa kuwa nuru yako imekuja,
Na utukufu wa Bwana umekuzukia

1 comment:

  1. Godbless you servant of God have been blessed.

    ReplyDelete