m

"If you want to conquer fear, don't sit at home and think about it. Go out and get busy. "

-- Dale Carnegie, motivational expert

Tuesday, 28 May 2013

MSITU WA TANESCO SAE MBEYA NI HATARI

TANESCO wanapaswa kufikiri zaidi ili kuwanusuru wakazi wa Sae na maeneo ya jirani wanaokatiza kwenye msitu wa Tanesco kutokana na kukithiri kwa vibaka. Kila jioni wakazi wa eneo hilo wamekuwa na hofu ya usalama wao na mali zao, hivyo kuomba msitu huo uondolewe. 

Kama inaonekana msitu huo kuwa muhimu basi wapange walinzi wa zamu kulinda ndani ya msitu huo ili kutoruhusu vibaka kufanya maficho kwa ajili ya kuvizia watu wanaopita nyakati za jioni.







Mbunge amlipua Blandina Nyoni

*Ni Katibu Mkuu wa zamani Wizara ya Afya
*Adaiwa kuchakachua mashine ya kusafisha figo
*Aelezwa aliiitoa Muhimbili kuipeleka Aga Khan

MBUNGE mmoja amemlipua aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni akidai alishiriki kuhamisha mashine ya kusafisha figo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Akiuliza swali bungeni jana, Mbunge wa Viti Maalum, Magdalena Sakaya (CUF) alidai Katibu Mkuu huyo kwa kushirikiana na daktari katika hospitali hiyo walihamisha mashine hiyo na kuipeleka katika Hospitali binafsi ya Aga Khan.“

Lini Serikali itairudisha mashine ya kusafisha figo iliyohamishwa kutoka Muhimbili na aliyekuwa Katibu Mkuu kwa kushirikiana na daktari wa hospitali hiyo na kuipeleka katika Hospitali ya ‘private?’, alihoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid alisema asingeweza kujibu swali hilo kwa kuwa hakuwa na taarifa kamili.

Anguko la elimu; cha kufanya kujinasua (3)

Share bookmark Print Email Rating
 
Na John Malata  (email the author)

Posted  Jumanne,Mei28  2013  saa 14:57 PM
Kwa ufupi
  • Serikali kwa nyakati tofauti imejaribu kuweka msisitizo wa ufundishaji kwa kutumia lugha ya Kiingereza bila mafanikio. Mfano mzuri ni mradi ujulikanao kwa jina la English Language Teaching Support Project 1996-2000 (ELTSP).

Leo nahitimisha mfululizo wa makala zangu kuhusu sababu za anguko la elimu nchini na namna tunavyoweza kunusuru mustakbali wa elimu yetu. Endelea…
Serikali kwa nyakati tofauti imejaribu kuweka msisitizo wa ufundishaji kwa kutumia lugha ya Kiingereza bila mafanikio. Mfano mzuri ni mradi ujulikanao kwa jina la English Language Teaching Support Project 1996-2000 (ELTSP).
Mradi huu ni miongoni mwa mikakati iliyoshindwa kutuletea manufaa katika ufundishaji wa lugha ya Kiingereza shuleni kama lugha ya kufundishia. Ifike wakati tukubali sasa kuwa tunahitaji kufanya uamuzi mgumu na wenye gharama kwa manufaa ya taifa letu.
Idara ya Ukaguzi ndicho chombo chenye mamlaka ya kusimamia ubora wa elimu itolewayo nchini. Hata hivyo, idara hii imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi, jambo linalosababisha ishindwe kutimiza wajibu wake ipasavyo.
Kuna haja ya kudurusu upya majukumu ya idara hii ili pamoja na mambo mengine, miongozo na mipango katika ukaguzi wa shule itoe kipaumbele katika matokeo ya wanafunzi.
Ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2008, inaeleza wazi kuwa ukaguzi shuleni umeshindwa kusimamia utoaji wa elimu bora.
Kuna haja ya Serikali kuangalia uwezekano wa kuifanya idara ya ukaguzi wa shule kuwa taasisi inayojitegemea kama zilivyo taasisi nyingine za elimu. Aidha, muundo na utendaji wake viangaliwe upya ili kuipa nguvu idara hii.
Ninaamini idara hii ikiwezeshwa kwa kupewa hadhi ya kuwa taasisi au hata mamlaka kamili, upo uwezekano mkubwa kuwa sasa shule zetu zitakuwa na nafasi kubwa ya kukaguliwa mara kwa mara. Kwa hakika tunahitaji kuwa na shule zinazokaguliwa.
Wajibu wa wadau wa elimu
Katika muktadha wa mjadala huu, wadau wa elimu ni pamoja na waajiri, wazazi, walimu na wanafunzi. Kila mmoja kati ya hawa ana wajibu wa kujenga mustakabali wa maendeleo ya Taifa, kwa kuhakikisha anatimiza wajibu wake kikamilifu.
Mwajiri kwa mfano, anapaswa kuhakikisha kuwa mwalimu anajengewa uwezo na mazingira bora yatakayo mwezesha kutekeleza wajibu wake akiwa na moyo mkunjufu.
Aidha, wazazi na jamii kwa jumla ni kiungo muhimu sana katika kuinua kiwango cha elimu hapa nchini. Hii inatokana na ukweli kuwa mwanafunzi ni zao la jamii husika na ndiko anakotumia muda mwingi katika ukuaji wake nje ya shule.
1 | 2 Next Page»
http://www.mwananchi.co.tz/uchambuzi/Anguko-la-elimu--cha-kufanya-kujinasua--3-/-/1597604/1865152/-/lw5nhsz/-/index.html

Sudan yatisha kufungia Sudan.K mafuta

Rais Omar el Bashir
Rais wa Sudan Omar al-Bashir ametishia, kufunga kabisa bomba la mafuta ambalo husafirisha mafuta kutoka Sudan Kusini hadi pwani ya Sudan, Red Sea.
Alisema kuwa Sudan itasitisha usafirishwaji wa mafuta ikiwa Sudan Kusini haitakoma kuwaunga mkono waasi wanaoendesha harakati zao katika eneo la mafuta la Sudan.
Jeshi la Sudan linapambana na waasi katika angalao maeneo matatu ya nchi hiyo.
Licha ya Sudan Kusini kujitawala mwaka 2011, hali ya wasiwasi kuhusu mafuta na ardhi imekuwa ikiendelea.
''Na sasa natoa onyo la mwisho kwa ndugu zetu wa Sudan Kusini kuwa tutafunga kabisa bomba la mafuta ikiwa wataendelea kuunga mkono wasaliti katika jimbo la Darfur , Kordofan ya Kusini na Blue Nile'' alisema Bashir kupitia televisheni ya taifa huku akigusia waasi wanaoendesha harakati zao katika maeneo hayo.
Kundi la waasi lenye mirengo mingi, linalojulikana kama Sudan Revolutionary Front (SRF), limefanya mashambulizi katika miji kadhaa huku wakiteka mji mkubwa wa Um Rawaba , katikati mwa Sudan mwezi Aprili.
Kundi hilo linalonuia kuipindua serikali ya rais Bashir, lakini wakaendelea kudhibiti mji wa Abu Kershola, katika eneo jirani la Kordofan Kusini.
Waasi wa SPLM-North walijiunga na kundi la waasi la JEM kutoka Darfur pamoja na makundi mengine ambayo ni ya mrengo wa (SLA), kwa lengo la kubuni kundi la
Sudan Revolutionary Front mwaka jana.
Rais Bashir alitoa hotuba yake moja kwa moja kupitia televisheni ya taifa nchini Sudan, kufuatia tangazo la jeshi kuwa limeweza kuteka tena mji wa Abu Kershola kutoka kwa waasi.
Wakati huohuo, msemaji wa waasi hao aliambia shirika la habari la AFP kuwa wapiganaji waliondoka kutoka, eneo la Abu Kershola ili kulegeza vikwazo vya serikali kwa wenyeji wa eneo hilo.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umekuwa ukitetereka tangu mwaka 2011, wakati Sudan Kusini ilipoamua kujitawala.
Maswala muhimu kuhusu Uzalishaji wa mafuta, mizozo ya mipaka ynagali kutatuliwa.
bbcswahili

Kongo yagawika pendekezo la Kikwete

Pendekezo la Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo izungumze na makundi ya waasi na nchi jirani kutatua mzozo wa mashariki ya nchi hiyo linaonekana kuwagawa Wakongo.
Kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa, kuna mwangwi wa sauti za Wakongomani wakiupongeza msimamo wa Rais Kikwete kwamba kuweko na mtazamo wa ujumla katika kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa kanda ya Maziwa Makuu.
Mwandishi wetu wa Kinshasa anaripoti kwamba wakaazi wengi wa mji huo wanaamini kuwa pendekezo hilo la Rais Kikwete linaweza kusaidia amani ya kudumu.
Kwenye mkutano wa marais 11 wa Nchi za Maziwa Makuu kwa ajili ya Kongo uliotishwa kando ya mkutano wa Umoja wa Afrika, mjini AddisAbaba, Rais Kikwete alipendekeza kufanyike mazungumzo baina ya Kongo na kundi la waasi la M23, Rwanda na kundi la waasi la FDLR na Uganda na waasi wake wa ADF/Nalu kwa ajili ya amani ya kudumu ya kanda ya Maziwa Makuu.
Tanzania inachangia wanajeshi 1,280 kwenye kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa mashariki mwa Kongo,
Umoja usio wa kawaida Kinshasa
Rais Paul Kagame wa Rwanda (kushoto) na Joseph Kabila wa DRC. Rais Paul Kagame wa Rwanda (kushoto) na Joseph Kabila wa DRC.
Pendekezo hili limezua kile mwandishi wetu wa Kinshasa anachokiita “tukio la nadra kabisa nchini Kongo“ kwa wabunge wa upinzani na wale wa chama tawala kuwa na kauli moja kuhusu maswala muhimu ya kitaifa.
Rais Kikwete amefanikiwa kuwaelekeza wanasiasa wa Kongo kuchukuwa msimamo wa pamoja kuhusu juhudi za kutafuta suluhisho la kudumu kwenye kanda ya Maziwa Makuu.
Kwa mujibu wa taarifa za mashirika ya habari ni kwamba Rais Kikwete aliwambia maraisi wenzake pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Afrika, kwamba ni lazima kuweko na mtizamo wa ujumla kwa ajili ya kumalizisha machafuko ya miaka mingi kwenye kanda la Maziwa Makuu.
Kwa hiyo Rais Kikwete alipendekeza Kongo kuendesha mazungumzo na waasi wa M23, na vilevile kuitaka Rwanda kuzungumza na waasi wa FDLR na Uganda kufungua mazungumzo na waasi wake wa ADF/Nalu. Pendekezo hilo limepongezwa na upinzani na chama tawala nchini Kongo, akiwemo mbunge Justin Bitakwira, ambaye ni kiongozi wa wabunge wa upinzani wa UNC.
Naye Franklin Tshamala, msemaji wa muungano wa vyama tawala, amesema kwamba pendekezo hilo la Rais Kikwete ni hatua ya ujasiri ya kutaka kurekebisha mitizamo tofauti waliyonayo viongozi wa mataifa haya matatu.
Rwanda yakataa
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC. Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC.
Pendekezo hilo la Rais wa Tanzania lilipongezwa pia na serikali ya Kongo. Akiwa mjini Addis Ababa, Waziri wa Mambo ya Nje ya Kongo, Raymond Tshibanda, aliiambia Radio France Internationale kwamba msimamo huo unalingana na ombi la miaka mingi la serikali ya Kongo kwa majirani zake.
Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo, aliyehojiwa na redio hiyo hiyo alisema matamshi hayo ya Rais Kikwete ni ya upotofu na nchi yake haiwezi kamwe kuzungumza na watu waliohusika na mauwaji ya halaiki.
Magazeti mengi ya siku ya Jumanne (tarehe 28 Mei) yamezungumzia matamshi ya Rais Kikwete na maoni ya wananchi wa Kongo. Gazeti Lavenir limechapisha kichwa cha habari kwa wino mzito kikimuita Rais Kikwete ”Jjasiri wa kanda ya Maziwa Makuu.”
Kwenye ukarasa wa mwanzo, gazeti la upinzani la Tempetes des Tropiques limeandika “Kikwete arusha bomu Addis Abeba”, likiyaelezea matamshi ya Rais Kikwete kuwa sawa na bomu alilowarushia marais wenzake ambao kwa muda mrefu wameonyesha unafiki katika kumaliza machafuko ya Maziwa Makuu kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Goma hawataki mazungumzo na M23
Wakimbizi wa ndani mashariki ya Kongo. Wakimbizi wa ndani mashariki ya Kongo.
Lakini hali ikiwa hivyo mjini Kinshasa, kwenye eneo la mashariki ya Kongo, ambako ndiko hasa kwenye mgogoro kati ya serikali na waasi wa M23, maoni ni tafauti.
Mwandishi wetu wa Goma, John Kanyunyu, anaripoti kwamba mashirika ya kiraia ya huko yamekataa mazungumzo baina ya serikali ya DRC na wajumbe wa M23.

Makamu mwenyekiti wa mashirika ya hayo kiraia katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, ambaye pia ni msemaji wa mashirika hayo, Omar Kavota, amesema “hakuna tena la kuzungumza, kwani tayari mkataba wa M23 baina ya chama cha zamani cha uasi CNDP umeshajadiliwa.”

Kauli hiyo ya mashirika ya kiraia inakuja baada ya pendekezo la Rais Kikwete mbele ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na marais wa kanda ya Maziwa Makuu kuiomba serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo baina yake na waasi wa M23.
Aidha kauli hiyo ya mashirika ya kiraia ya kuitaka serikali kutozungumza na wajumbe wa M23, inachochewa pia na utendaji kazi wa wanajeshi wa serikali katika uwanja wa mapigano.

Katika vita baina ya jeshi la serikali, FARDC, na waasi wa M23, jeshi hilo la serikali linatajwa kuwa, lilifaulu kwa mara ya kwanza kabisa, kuwazuia waasi wa M23 kuuteka upya mji wa Goma.

Kavota anasema ni bora zaidi kuwapatia nafasi ya kufanya kazi zao wanajeshi wa kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa kinachowajumuisha wanajeshi kutoka Tanzania, Malawi na Afrika ya Kusini.
Katika kuwapongeza wanajeshi wa serikali kwa kazi waliyoifanya wakati wa mapigano ya wiki iliyopita, mashirika ya wanawake kutoka asasi za kiraia na vyama vya kisiasa, wametoa mchango wa pesa wa kile walichokiita “kuwanunulia wanajeshi wa serikali maji ya kunywa.”
Ripoti hii imetayarishwa na Saleh Mwanamilongo, Kinshasa, na John Kanyunyu, Goma
Mhariri: Mohammed Khelef

DW.DE

Lagarde aepuka kushtakiwa

Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa Christine Lagarde Ijumaa (24.05.2013) aepuka kufunguliwa mashtaka mara moja lakini ametajwa kuwa "shahidi msaidizi" baada ya waendesha mashtaka wa Ufaransa kumhoji kwa siku mbili.
Lagarde alihojiwa kwa jumla ya saa 24 na waendesha mashtaka wa mahakama inayofanya uchunguzi wa kesi za wizara kwenda kinyume na taratibu wakati wa kushughulikia mzozo ambao umepelekea kulipwa kwa euro milioni 400 kwa mfanya biashara mwenye utata Bernard Tapie.Amewaambia waandishi wa habari wakati alipokuwa anatoka katika mahakama hiyo ya Paris Ijumaa usiku "Daraja aliyowekwa kuwa shahidi wa kusaidia haikumshangaza".
Lagarde mwenye umri wa miaka 57 amesema "daima amekuwa akifanya kazi kwa maslahi ya taifa na kwa mujibu wa sheria." Amekuwa akikanusha kwamba hakufanya kosa lolote lile na kwamba maelezo yake yamekuja kufuatia shaka zilizozuka kutokana na maamuzi aliyoyatowa wakati huo.
Wakati Lagarde ameweza kuepuka kuwekwa chini ya uchunguzi rasmi ambapo kwa daraja ya Ufaransa ni karibu sawa na kufunguliwa mashtaka, kuwa"shahidi wa kusaidia" kunamaanisha kwamba bado anaweza kukabiliwa na masuala zaidi na yumkini baadae akafunguliwa mashtaka.
IMF ina imani na Lagarde
Mkuu wa IMF Christine Lagarde akiwapungia watu walioko nje ya mahakama Ijumaa (24.05.2013) Mkuu wa IMF Christine Lagarde akiwapungia watu walioko nje ya mahakama Ijumaa (24.05.2013)
Lagarde amesema sasa anapaswa kurudi Washington Marekani na kuripoti kwa bodi ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambayo kwa mara nyengine tena imeelezea imani iliokuwa nayo kwa kiongozi wake wa kwanza wa kike baada ya kujuwa uamuzi huo wa mahakama.
Kwa Lagarde ambaye anahesabiwa kuwa miongoni mwa wanawake wenye sauti kubwa kabisa duniani alijipatia heshima wakati akiwa waziri wa kwanza wa fedha mwanamke nchini Ufaransa kwa msimamo wake wa kutotaka upuuzi,usomi na mtindo wake.
Mashtaka ya uhalifu dhidi ya mama huyo ingelikuwa ni karaha kwa IMF baada ya mtangulizi wake Dominique Strauss-Kahn ambaye pia anatokea Ufaransa kujiuzulu kwa idhara hapo mwaka 2011 kufuatia madai ya dhila ya ngono kwa mhudumu wa kike wa hoteli moja mjini New York.
Mkuu wa zamani wa IMF Dominique Strauss-Kahn. Mkuu wa zamani wa IMF Dominique Strauss-Kahn.
Msemaji wa IMF Gerry Rice amesema katika taarifa kwamba bodi ya utendaji itaarifiwa tena juu ya suala hilo hivi karibuni na kwamba bodi hiyo imekuwa ikiarifiwa mara kadhaa juu ya suala hilo na kila wakati imekuwa ikielezea imani yake kwa uwezo wa mkurugenzi wake huyo mtendaji kutekeleza kazi zake kwa ufanisi.
Uchunguzi huo unamhusisha Tapie mwanasiasa wa zamani ambaye aliwahi kufungwa gerezani kwa kupanga matokeo ya mechi wakati alipokuwa rais wa klabu ya soka ya Ufaransa ya Olympique de Marseille.
Waendesha mashtaka wa Mahakama ya Haki ya Jamhuri (CJR) walimtuhumu kupatiwa upendeleo ili aweze kumuunga mkono Rais Nicolas Sarkozy wakati wa uchaguzi wa rais wa mwaka 2007.Walidokeza kwamba Lagarde wakati huo akiwa waziri wa fedha alihusika kwa kiasi fulani na uvunjaji wa taratibu jambo ambalo lingeliweza kupelekea kufunguliwa mashtaka kwa kushiriki katika ulaghai na ubadhirifu wa fedha za umma.
Uchunguzi ulijikita juu ya hatua yake ya mwaka 2007 ya kulitaka jopo la majaji kusuluhisha katika mzozo wa kuuzwa kwa kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas hapo mwaka 1993 kati ya Tapie na Benki ya Mikopo ya Lyonnais iliosambaratika ambayo kwa kiasi fulani ilikuwa na umiliki wa serikali.Tapei aliishutumu benki hiyo kwa kumghilibu kutokana na kushusha thamani ya kampuni ya Adidas wakati wa kuuzwa kwake na kutaka serikali ikiwa mshika dau mkuu katika benki hiyo kumlipa fidia.
Mzozo ulikuwa wa gharama
Mfanyabiashara tajiri wa Ufaransa Bernard Tapie. Mfanyabiashara tajiri wa Ufaransa Bernard Tapie.
Hoja zake zilikubaliwa na jopo la usuluhishi lakini wahakiki wamedai kwamba serikali haikupaswa kutumbukizwa kwenye hatari ya kulazimishwa kulipa fidia kwa mtu aliepatikana na hatia ya uhalifu kwani wakati huo alikuwa amefilisika na asingeliweza kuiwasilisha kesi hiyo mahakamani.
Lagarde alisema usuluhishi huo ulikuwa ni muhimu kumaliza mzozo huo wenye gharama kubwa na daima amekuwa akikanusha kwamba alichukuwa hatua hiyo kwa kuamuriwa na Sarkozy.
Malipo aliyopokea Tapie yalimwezesha kulipa madeni yake makubwa na kodi ambapo kwa mujibu wa repoti za vyombo vya habari akibakiwa na euro milioni 20 hadi 40 ambazo alizutumia kuanzisha upya biashara.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri: Caro Robi
dw.de

Monday, 20 May 2013

Uvamizi kwa "kumfichua" Museveni


 20 Mei, 2013 - Saa 16:37 GMT

Ofisi za Gaeti la Daily Monitor zilizovamiwa na polisi wa Uganda
Polisi nchini Ugandan wamevamia ofisi za magazeti kufuatia taarifa kwamba Rais Yeweri Museveni anamuandaa mwanawe wa kiume kumrithi urais.
Vituo viwili vya Redio pia vamiwa na kuzimwa , hii ni kwa muujibu wa gazeti la serikali la New Vision.
Wiki iliyopita magazeti ya Uganda yalidai kuwa kuna njama za kuwaua wale watakao pinga mpango wa Rais Museveni kumuandaa mwanawe kuchukua madaraka ya Uganda.
Magazeti hayo yalidai kuwa mipango hiyo ya mauaji yalitolewa na Mkuu fulani wa jeshi la Uganda.
Bwana Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu 1986, anatarajiwa kung'atuka uongozini mwaka 2016.
Kwa muda mrefu kumekuwa na madai kwamba Museveni anamuandaa mwanawe Muhoozi Kainerugaba,ambaye ni brigadier jeshini kushikilia uongozi wa Uganda.
Lakini serikali ya Museveni imekanusha kwamba kuna mipango kama hiyo.

Mwanawe Museveni Brig. Kainerugaba.

Wiki iliyopita gazeti la, the Daily Monitor,na jengine la , Red Pepper, lilichapisha barua ya siri ikidai ilikuwa imeandikwa na Jeneral David Sejusa, ikitaka uchunguzi ufanywe kuthibitisha madai kwamba kuna mipango ya kuwauwa wote watakao piga mipango ya Rais Museveni kumpachika mwanawe uongozini.
Uvamizi huo wa polisi umeidhinishwa na mahakama ya Uganda na ulikuwa unalengo la kutafuta barua hiyo inayodaiwa kuandikwa na mkuu huyo wa Jeshi akifichua njama za mauaji.
Vituo viwili vya Redio vinavyohusiana na Daily Monitor, Dembe FM na KFM, pia vilivamiwa na kuzimwa.
Rais Yoweri Museveni
Mkurugenzi Mkuu wa Daily Monitor Bwana Alex Assimwe aliambia BBC kwamba Chumba chao cha Habari kilivamiwa na polisi wapatao 50 waliojihami kwa silaha.
Lakini wachanganuzi wa maswala ya kisiasa wanadai kuwa ikiwa barua ya Jenerali Sejusa ni ya kweli basi ni dalili kuwa kuna hali mvutano ndani ya jeshi huku ikidhaniwa kuwa wanajeshi wakongwe huenda wanapoteza uwezo kwa wanajeshi chipukizi wanaoongozwa na mwanawe Museveni Brigadia Kainerugaba.
Jenerali Sejusa ni mwanajeshi mkongwe aliyekuwa katika vita vya ukombozi uliyomuweka Rais Museveni madarakani mwaka1986.
Kwa muujibu wa taarifa za AP kamanda mmoja wa jeshi Jenerali Aronda Nyakairima amenukiliwa akisema kuwa Jenerali Sejusa kwa wakati huu anachunguzwa kutokana na barua anayodaiwa kuiandika.

Thursday, 16 May 2013

Tume ya Kidato cha IV yatoa mapendekezo 130

 
Profesa Sifuni Mchome 
Na Fredy Azzah, Mwananchi  (email the author)

Posted  Jumanne,Mei14  2013  saa 20:25 PM
Kwa ufupi
  • Pendekezo la kufutwa kwa matokeo na kisha kupangwa upya ni moja tu kati ya mengi. Mpaka sasa tumeandaa zaidi ya mapendekezo 130 na kazi bado inaendelea

Dar es Salaam. Tume ya Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha Ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012, imetoa mapendekezo 130, mojawapo ikitaka kupitiwa upya kwa mitalaa ya elimu nchini.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Profesa Sifuni Mchome alisema likitaka mitalaa ya shule za msingi hadi vyuo vya ualimu itazamwe upya.
Tume hiyo iliundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Februari 23, mwaka huu kuchunguza chanzo cha asilimia 65.5 ya wanafunzi kupata daraja la sifuri kwenye mtihani wa mwaka 2012.
Alisema mapendekezo hayo yatawasilishwa kwa Waziri Mkuu baada ya Tume kumaliza kazi yake Juni 15 mwaka huu.
“Pendekezo la kufutwa kwa matokeo na kisha kupangwa upya ni moja tu kati ya mengi. Mpaka sasa tumeandaa zaidi ya mapendekezo 130 na kazi bado inaendelea,” alisema Profesa Mchome.
Alisema kwa kawaida mtalaa unabadilishwa baada ya kumaliza mzunguko wake mmoja, hivyo tume hiyo imependekeza kupitiwa upya kwa mitalaa yote ambayo imemaliza mzunguko. Mzunguko huu ni miaka saba kwa elimu ya msingi, minne kwa sekondari na miwili kwa kidato cha tano na sita.
“Mtalaa wa sekondari unaweza kupitiwa upya baada ya miaka minne tangu kuanza kutumika kwake, huu wa Sekondari wa ‘based competence’ (kuangalia ubora) ulianza kutumika 2006, mpaka sasa tayari umemaliza mzunguko wake na haya matokeo yametokana na mtalaa huu.
Tume imependekeza mitalaa yote itazamwe upya kuanzia ile ya shule za msingi mpaka vyuo vya ualimu,” alisema.
Kuhusu vitabu, Tume imependekeza kuangaliwa kwa njia rahisi ya kutumia teknolojia kuhakikisha vinapatikana badala ya kusubiri mpaka vichapishwe na kisha kupelekwa kwa wanafunzi.
“Unaweza ukaongea na makampuni ya simu kuwa waweke vitabu kwenye system (mfumo) yao na wakaanza mashindano kuwa mwanafunzi atakayesoma sana atapata zawadi,” alisema na kuongeza.
“Unaweza pia kuongea na kampuni ya magazeti kama Mwananchi ukawaambia watoe ukurasa wachapishe kitabu fulani kwa mwezi mzima na shule ziambiwe zinunue nakala moja ambayo kwa mwezi itakuwa Sh30,000 kwa kila shule na tatizo la vitabu litakwisha.”
Pendekezo jingine alisema ni kuangaliwa upya kwa sheria mbalimbali za elimu jinsi zilivyo na utekelezwaji wake pamoja na kuhakikisha madaraka yanapelekwa kwenye ngazi za Serikali za Mitaa.
http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Tume-ya-Kidato-cha-IV-yatoa-mapendekezo-130/-/1597296/1852852/-/12p5ogez/-/index.html

Hayati Patrice Lumumba atunukiwa mji


Lumumba alichaguliwa kama waziri mkuu wa DRC mwaka 1960
Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo inatarejiwa kujenga mji ambao utakuwa kumbukumbu na kwa mpiganiaji uhuru wa nchi hiyo Patrice Lumumba . Hii ni kwa mujibu wa msemaji wa serikali Lambert Mende.
Lumumba aliongeza kuwa, mji huo utakaojulikana kama Lumumbaville utazileta pamoja jamii mbili zilizoko katika eneo hilo.
Lumumba aliyekuwa mshirika wa nchi za muungano wa Kisovieti, alichaguliwa kama waziri mkuu mwaka 1960, baada ya zaidi ya karne moja ya utawala wa kikoloni.
Mauaji yake, yalitokea miezi minne baadaye alipokuwa na umri wa miaka 35 na Marekani na Uingereza ndizo zililaumiwa kwa kifo chake.
Mwezi Aprili, mmoja wa wabunge wa bunge la malodi nchini Uingereza alisema kuwa afisaa mmoja wa MI6, alimwambia kuwa Uingereza ilihusika na kifo cha Lumumba.
Mwandishi wa BBC mjini Kishansa anasema kuwa habari hii bila shaka itapokelewa vyema na wananchi wa DRC kwani Lumumba anasalia kuwa mtu mashuhuri.
Mji wa Lumumbaville utajengwa katika mkoa wa Kassai-Oriental ambako alizaliwa hayati Lumumba.
Ujenzi wa mji huo unatarajiwa kuanza mwaka 2014, aliongeza kusema bwana Mende.
Serikali inatumai kuwa wahisani watasaidia katika ujenzi wa mji huo na kuwa utakuwa kivutio kwa watalii.
Mwanawe Lumumba, Raymond, aliambia BBC kuwa babake angefurahia sana uamuzi wa serikali kujenga mji huo.
"alitaka Congo kuwa kitovu cha maendeleo barani Afrika," alisema Raymond Lumumba.
"kwa hivyo, angetaka uwe mji wa kisasa.''
DR Congo ina utajiri wa madini ingawa watu wengi wanaishi katika umaskini.
Nchi hiyo imekumbwa sana na mizozo kadha wa kadha tangu ijipatie uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.
Mzozo wa hivi sasa ambao umesababishwa na kundi la M23, ulianza mwaka jana Mashariki mwa nchi na kusababisha takriban watu 800,000 kutoroka makwao.
chanzo; bbcswahili.com

Tuesday, 7 May 2013

DRC: Nchi hatari zaidi kwa mama

Shirika la kimataifa la kuhudumia watoto - Save the Children limeitaja Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuwa eneo baya zaidi ulimwenguni kuishi ukiwa mama, wakati Finland ikiibuka eneo bora zaidi.
Shirika la kimataifa la kuhudumia watoto - Save the Children limeitaja Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuwa eneo baya zaidi ulimwenguni kuishi ukiwa mama.
Ripoti ya shirika hilo lenye makao yake jijini London Uingereza iliyotolewa leo inaonyesha kuwa mataifa ya kiafrika yemechukua nafasi zote kumi za chini kabisaa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 14 wakati Finland na nchi nyengine za Skandinavia zikiongoza  katika kumi bora.
Nembo ya shirika la Save the Children Nembo ya shirika la Save the Children
Ripoti hiyo iliyopewa kichwa cha 'Hali ya kina mama wa dunia' inalinganisha mataifa 176 kwa kuizingatia vitu kama afya ya uzazi, vifo vya watoto, elimu na viwango vya mapato ya wanawake na hadhi zao za kisiasa. Save the Children ilitoa wito wa kupunguza tofauti kubwa katika upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi kati ya mataifa yaliyoendelea na yale yanayoendelea, na kuwepo na juhudi za maksudi kupambana dhidi ya ukosefu wa usawa na utapiamlo.
Ripoti hiyo imegundua kuwa mwanamke au msichana yuko katika hatari zaidi ya kufariki kutokana sababu zinazohusiana na uzazi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa nafasi moja katika 30, hii ikiwa ni pamoja na wakati wa kujifungua, ikilinganishwa na nchini Finland, ambako hatari hiyo ni nfasi moja katika 12,200.  Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Save the Children Jasmine Whitehead, alisema kwa kuwekeza kwa kina mama na watoto, mataifa yatakuwa yanawekeza katika mafanikio yao ya baadae.
Elimu kwa wanawake itasaidia ustawi wao na wa watoto
Amesema kama wanawake wanaelimishwa, wanawakilishwa kisiasa, na wanapata huduma nzuri za afya ya uzazi na huduma za watoto, basi kuna uwezekano mkubwa kwa wao na watoto wao kuishi vizuri na kustawi , na hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa jamii wanamoishi. Alisema kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mataifa yanaoyoendelea, lakini kazi bado kuna kazi kubwa inayotakiwa kufanywa ili kuokoa na kuboresha mamilioni ya maisha ya kina mama maskini zaidi na ya watoto wanaozaliwa.
Wanawake nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wakisubiri maji mjini Kinshasa.  
Wanawake nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wakisubiri maji mjini Kinshasa.
Baada ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, mataifa yanayofuatia kwa kuwa hatari zaidi kwa kina mama yaliorodheshwa kuwa ni Somalia, Sierra Leon, Mali na Niger. Ripoti hiyo inasema viwango vikubwa vya vifo vya watoto katika bara la Afrika chini ya jangwa la Sahara, vinatokana na afya duni ya kina mama -- ikionyesha tarakimu zinazoonyesha kuwa asilimia kati ya 10 na 20 wako chini ya uzito unaotakiwa.
Ripoti hiyo pia ilitoa umuhimu kwa idadi ya kina mama wanaojifungua kabla watoto wao hawajakua, matumizi madogo ya vizuia mimba, upatikanaji mdogo wa huduma za afya ya uzazi na uhaba wa wafanyakazi wa afya. Mataifa ya juu baada ya Finland ni Sweden, Norway, Iceland na Uholanzi, wakati Marekani ikishika nafasi ya 30 nyuma ya Slovenia na Lithuania.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

FBI watua Arusha kusaka magaidi

 7 Mei, 2013 - Saa 11:24 GMT

Makachero wa FBI wawasili Mjini Arusha kusaidia Polisi Tanzania kusaka magaidi
kachero wa FBI kutoka Marekani wamewasili nchini Tanzania kusaidia katika upelelezi wa shambulizi la bomu lililotekelezwa katika kanisa katoliki mjini Arusha siku ya jumapili.
Mwandishi wa BBC Baruan Muhuza akiwa mjini Arusha anasema makachero hao wa FBI wako Tanzania kusaidiana na Jeshi la wananchi wa Tanzania na Polisi kutafuta undani wa tukio hili ambalo limeishtua na kuiweka serikali ya Tanzania katika wakati mgumu.
Baruan Muhuza anaongezea hali inaonekana kuwa ngumu zaidi hasa kutokana na aina ya matukio ambayo yamekuwa yakitokea katika siku za hivi karibuni yakihusisha viongozi wa dini ambapo wengi ya wanaodhurika huwa ni wa imani ya kikristo.
Wakati huo huo wakuu wa serikali wakishirikiana na viongozi wa kidini wameandaa mkutano utakaojumuisha viongozi wapatao 200.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiq amewaambia wanahabari kuwa wamelazimika kuandaa mkutano huo wa siku mbili kufuatia agizo la Rais Jakaya Kikwete.
Mkutano huo utajadili uhusiano bora baina ya wakrito na waislamu.
bbcswahili.com

Monday, 6 May 2013

MFANYA BIASHARA ALIYEJIRUSHA TOKA GOROFA YA TISA AFARIKI DUNIA

TAARIFA za awali zina arifu kuwa Mfanya Biashara, Costa Shirima anaedaiwa kujirusha kutoka gorofa ya tisa ya Hoteli ya Concord iliyopo Kariakoo Jijini Dar es Salaam inaelezwa kuwa alikuwa asafiri na ndege ya saa 10 jioni kuelekea China kufuata bidhaa za maduka yake.
Shirima (47), ambaye amefikwa na umauti muda mfupi baada ya kudondoka chini ni mfanyabiashara aliyekuwa akimiliki maduka kadhaa ya urembo wa akina mama yaliyopo jirani na Hoteli hiyo ya Concord.
Aidha taarifa hizo za awali kutoka kwa mmoja wa wanafamilia ambaye alidai kuwa si msemaji wa familia ya Shirima ya Mwika Moshi mkoani Kilimanjaro, nikuwa Marehemu mara kwamara alikuwa akipendelea kula katika hoteli hiyo na siku ya tukio inadaiwa kuwa aliwaeleza watu kuwa anapanda juu ya Hoteli hiyo kupunga upepo baada ya kuhisi hewa nzito mahali alipokuwa.
Inadaiwa kuwa baada ya kupanda huko juu ghafla alianguka chini na kudondokea gari dogo aina ya Toyota Corola linalofanya biashara ya Taxi na kupoteza maisha yake na gari hilo kuharibika vibaya kutokana na kishindo hicho.
Marehemu Shirima mbali na kuwa Mfanya Biashara wa muda mrefu Kariakoo pia alikuwa akiendelea na Ujenzi wa Jengo la Gorofa maeneo ya Kariakoo.
Marehemu ameacha Mjane na watoto 5.
Uchunguzi wa Kipolisi bado unaendelea kuhusiana na tukio hilo na taarifa kamili zitatolewa pindi zitakapo kamilika

Mfanya biashara huyu mkazi wa Dar es salaam mzaliwa wa Moshi kilimanjaro alikutwa na mauti hayo baada ya kujirusha kutoka gorofa ya tisa ya hoteli hiyo ambayo alienda kwa lengo la kuuona ukumbi wa tukio hilo ambao uko gorofa ya tisa ya hoteli hiyo.
Chanzo Cha Mfanyabiashara huyu kujirusha bado hakijafahamika mpaka sasa.
Taratibu za Mazishi ya Marehemu Zinapangwa jijini dar es salaam  na tukizipata tutakuhabarisha mapema. 
Ndugu Costa shirima ameacha mke na watoto.
Mungu ailaze roho ya marehemu Mahali Pema Peponi 
Amina
chanzo;jambotz